DR.MVUNGI AFARIKI DUNIA

November 12, 2013
DAR ES SALAAM, Tanzania

MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Dk. Sengondo Mvungi (61), amefariki dunia leo majira ya mchana katika hospitali ya Milpark, nchini Afrika Kusini alipopelekwa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Dk, Mvungi alivamiwa Novemba 3 mwaka huu na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi saa 6:30 usiku nyumbani kwake Kibamba, Kata ya Mpiji Majohe nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kujeruhiwa kwa mapanga sehemu za kichwani na usoni.

Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa hizo na kuwa chama hicho kimepoteza kiongozi makini na pengo lake haliwezi kuzibika.

“Ni kweli tumepata taarifa hizo mwenzetu hatunaye tena ni huzuni kwa chama na Watanzania tutamkumbuka kwa mambo mengi ndani ya chama hata taifa,” alisema.

Alisema kuwa Dk Mvungi alifariki dunia jana saa 9:30 katika hospitali hiyo ambapo alihamishiwa Novemba 8 mwaka huu akitokea katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).

Naye Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo Dk Mvungi.


Mbowe alisema kuwa Chadema kinatoa pole kwa familia, chama cha NCCR-Mageuzi, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na Watanzania wote kwa kupoteza mtu makini na muhimu katika mustakabari wa taifa letu.

“Nimepokea taarifa hizo kwa masikitiko kwa kuwa Dk Mvungi ni mmojawapo ya waasisi wa mageuzi nchini, ambaye hakukata tamaa kutumia taaluma yake Mungu ana mipango yake, huyu ndugu alijitahidi kupigania suala la Katiba mpya kwa miaka 20, na akateuliwa aiandae, tunasikitika kwa kuwa hataona katiba mpya yenye mawazo yake,” alisema.


Alisema kuwa Tume inapaswa kuendeleza mawazo na michango aliyokuwa akisaidia katika kuandaliwa kwa katiba mpya.


Aidha taarifa za kifo cha mwanasheria huyo ilisambaa kwa kasi katika mitandao mbalimbali ya kijamii, huku wadau wa mitandao hiyo wakionekana kushitushwa na kifo hicho na kuwataka Watanzania kuwa na subira kwa wakati huu mgumu.

Aidha Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hussein Bashe katika ukurasa wake aliandika kuwa wahalifu wamekatisha uhai wa kiongozi huyo wakati akitekeleza jukumu zito la kwa ajili ya maslai ya Taifa letu. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,” alisema Bashe.


Source:Habarimsetoblog

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »