COASTAL UNION YAWAKATA MAINI JAMHURI YA PEMBA.

November 08, 2013
Na Masanja Mabula -Pemba .
Uongozi wa klabu ya Coastal Union ya Tanga umewakata maini mashabiki wa timu ya Jamhuri juu ya usajili wa wachezaji wake Abdalla Othman na Suleiman Kassim Selembe  wakati wa dirisha dogo na kusema kuwa wachezaji hao  wataendelea kuitumikia klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya Vodacom .

Mwenyekiti wa klabu  hiyo Hemed Aurora  ameliambia blog hii kuwa taarifa za wachezaji hao kudaiwa kujiunga na timu ya Jamhuri kwa mkopo wakati wa dirisha dogo hazina ukweli na kuongeza kwamba wachezaji hao ni muhimu na wanawahitaji katika mzunguko wa pili ya ligi hiyo .

Amesema kuwa wachezaji hao bado ni muhimu kwenye kikosi cha timu hiyo , na kwamba mpango wa kuwatoa kwa mkopo haupo na badala yake wanaangalia kuongeza wachezaji kuziba mapengo yaliyojitokeza katika msunguko wa kwanza ulimalizika wiki hii .

"Taarifa hizo hazipo kwenye klabu yetu , tunajua wachezaji hawa ni muhimu na bado tunawahitaji , hivyo mpango wa kuwatoa kwa mkopo haupo na lwa sasa tunaangalia mbele kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kwenye msunguko wa kwanza " alieleza .

Aidha amefahamisha kuwa kamati Tendaji ya klabu hiyo inatarajia kufanya kikao mwishoni mwa wiki hii , ambapo ajenda itakuwa ni kujadili mwenendo wa timu kwenye ligi kuu pamoja na kupitisha jina la kocha atakayechukua nafasi iliyoachwa wazi na Hemed Moroco .

"Tumepokea maombi ya makocha wanne , ambapo kati yao  wawili kutoka nje ya nchi na wawili ni wazalendo , kamati tendaji itakutana na kupitia vielelezo vyao ili kupata kocha atakayeiongoza timu kwenye duru la pili la ligi hapo mwakani " alifahamisha .

Kabla ya hapo kulikuwepo na taarifa ambazo zinawahusu wachezaji hao kujiunga na Timu ya Jamhuri wakati wa dirisha dogo la usajili ili kuiongezea nguvu timu hiyo ambayo ushiriki wake kwenye ligi kuu ya Zanzibar ni wa kusuasua .

Taarifa hizo zitazidisha machungu kwa mashabiki wa timu wa timu ya Jamhuri ambao walikuwa wameanza kushusha presha  kuwa timu yao imepata wachezaji ambao watasaidia kuinasua na wimbi la kushuka daraja .

"Taarifa hizi zimezidi kutuumiza kwani tulikuwa na furaha kwamba wachezaji hao wawili wangetua kikosi cha timu yetu kingekuwa kimeiimarika " alisema shabiki wakati alipozungumza na mwandishi wa habari hizi .

Timu ya Jamhuri ndiyo inayoshika mkia wa ligi kuu ya Zanzibar kwa kuwa na alama tatu baada ya kushuka uwanjani mara  11 .

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »