KAMATI YA WANAWAKE, TWFA YAPONGEZWA

October 07, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) wamepongezwa kwa kuhakikisha akina mama wanacheza mashindano mbalimbali.

Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambapo amesema timu za wanawake zimekuwa zikishiriki katika mashindano mbalimbali licha ya ukweli kuwa hadi sasa hakuna udhamini kwenye mchezo huo.

Amesema mpira wa miguu unaendeshwa na udhamini na kuchangia, jambo ambalo linafanikishwa kwa kiasi kikubwa na uwazi katika matumizi ya fedha, jambo ambalo hivi sasa lipo ndani ya TFF.

Rais Tenga amesema baada ya kuanzisha Kamati ya Ligi, hivi sasa TFF inapata asilimia 4.5 tu ya mapato ya mechi za ligi kutoka asilimia 33 iliyokuwa ikipata wakati anaingia madarakani mwaka 2004.

Amesema asilimia hiyo 4.5 haiwezi kuendesha mpira na ndiyo maana nguvu zinaelekezwa katika kutafuta wadhamini na kuchangia. Pia TFF inatoa zaidi ya asilimia 15 ya Fedha za Msaada wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FAP) kutoka FIFA kwenye mpira wa miguu wa wanawake ambapo ni nchi chache zinazofikia kiwango hicho.

Hivyo, ametoa mwito kwa kampuni kujitokeza kudhamini au kuchangia timu za Taifa za mpira wa miguu za wanawake ambazo zinashiriki mashindano mbalimbali mwaka huu, kwani gharama za kuziendesha ni kubwa.

Timu ya wakubwa (Twiga Stars) inacheza mashindano ya mchujo ya Fainali za Afrika (AWC) zitakazofanyika mwakani nchini Namibia wakati ile ya chini ya miaka 20 inacheza mashindano ya Dunia ambayo fainali pia zitachezwa mwakani nchini Canada.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »