DC Mgaza awahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya afya.

April 24, 2013
 Na Oscar Assenga,Mkinga. 
MKUU wa wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza amewataka wazazi na walezi wilayani humo kuhakikisha wapeleka watoto wanaostahili chanjo katika vituo vya huduma za afya ili kuwazuia wasipatwe na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya milipuko
Wito huo aliutoa leo wakati wa uzunduzi wa wiki ya chanjo iliyofanyika katika kituo cha Afya Gombero ambapo alisema kila mzazi anapaswa kuhakikisha mtoto wake na wa jirani yake ambayo hajapata chanjo anapewa haki yake ya msingi ya kupatiwa huduma hiyo
Mgaza alisema baada ya kuzindua huduma hiyo anaimani kuwa wazazi watawapeleka watoto wao katika vituo vya kutolea huduma hiyo ambayo itatolewa wilayani humo kuanzia leo (jana) mpaka mwishoni mwa wiki.
Aidha alitumia nafasi aliyopata wakati akiwahutubia wananchi waliojitokeza kwwenye uzinduzi huo kwa kuwakumbusha kuhusu chanjo mpya za kuwakinga watoto na ugonjwa wa nimonia, kuhara na homa ya uti wa mgongo zilizoanza kutolewa tokea mwazoni mwa mwaka huu.
Alisema kuwa chanjo hizo ni haki ya kila mtoto mwenye umri chini ya mwaka mmoja hivyo zitaongeza kasi ya kupunguza vifo kwa walengwa na kusisitiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata chanjo zote kwa kufuata ratiba.
Aidha alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana lakini bado zipo changamoto ya kuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo au hawajakamilisha chanjo kutokana na umri wao.
Alieleza watoto hao wako katika hatari kubwa kupata maambukizo ya magonjwa na kuweza kuhatarisha jamii nzima na kueleza ni muhimu sana kwa kila mzazi na mlezi kuhakikisha wanawapatia watoto wao chanjo zote kila wakati,ili kuwadhibiti na magonja mfano polio na surua hasa ukizingatia kumekuwepo na mlipuko wa polio katika nchi jirani.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa huduma ya chanjo katika wilaya hiyo, Mratibu wa Chanjo wilaya ya Mkinga, Aisibo Maimu alisema huduma ya chanjo wilayani humo inatolewa kwenye vituo vya afya 26 vikiwemo vituo vya afya vitatu, zahanati 23 za serikali na zahanati moja ya Mtimbwani ambayo ni ya faith Based Organization (FBO) ambapo pia huduma za chanjo zimekuwa zikitolewa kwa njia chanjo wima katika vijiji 35 na chanjo mkoba katika vijiji 5 wilayani humo.
Aidha amesema pamoja na mafanikio yaliyopo lakini pia zipo changamoto katika utoaji wa huduma hiyo kwa baadhi ya watoto wanaozaliwa, kucheleweshwa na wazazi wao kupata chanjo 0 kutokana na mama zao kujifungulia nyumbani.
Ameongeza kuwa changamoto nyengine ni miundo mbinu ya barabara kuwa tatizo hasa maeneo ya Mkota na Ronjo katika kata ya Mwakijembe ambapo idadi kubwa ya jamii ya wafugaji wanaishi humo.
Hata hivyo amesema idara ya afya wilayani humo haijakaa kimya, bado inaendelea kuhamasisha kina mama kujifungulia katika vituo vya afya ili wapate huduma pamoja na haki zao za msingi ikiwemo chanjo ya polio.
Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »