DC Mwanga apiga marufuku Lambalamba”

April 24, 2013

 


Na Oscar Assenga,Lushoto.
 
MKUU wa wilayani Lushoto Mkoani Tanga,Alhaj Majid Mwanga imepiga marufuku vikundi vya waganga wanaofanya shughuli za kufichua wachawi maarufu kama “Lambalamba” wilayani humo pamoja na kutoa tahadhari kwa wanannchi watakaobainika kushirikiana nao watachukuliwa hatua kali.

Agizo hilo la Mwanga alilitoa jana kutokana na kutokea uharibifu mkubwa katika kituo cha polisi Bumbuli pamoja na Ofisi ya Afisa Mtendaji tarafa hiyo uliofanywa na wafuasi wa lambalamba waliovamia kituo hicho na kuvunja kila kitu kilichokuwemo ndani ikiwemo nyaraka zote muhimu za serikali na kumchomoa mhalifu mmoja aliyekuwa amewekwa kituoni hapo.

Mwanga alisema baada ya wafuasi hao kumaliza wakaamia ofisi ya afisa tarafa ambapo walifanya uharibifu mkubwa ikiwemo kuchana nyaraka ,thamani za ofisi zilizokuwemo ndani yake.
Alisema baada ya kufanyika matukio hayo hatua ya kwanza walihakikisha usalama katika eneo hilo unakuwepo kwa asilimia kubwa na baadae kuanza kuwasaka waliohusika na tukio hilo ambalo lilikwisha kupigwa marufuku muda mrefu.

Mkuu huyo wa wilaya alisema baada ya hapo walifanikiwa kuwakamata watu 32 ambao wanadhaniwa kuhusika na tukio hilo ambapo wanashikiliwa na jeshi la polisi wilayani humo na tayari walikwisha kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
   
“Napenda kuwaasa wananchi na madiwani kuacha kushirikiana na lambalamba au kuwafadhili katika maeneo yao kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na hatutawavumilia lazima wachukuliwe hatua stahiki ikiwemo kuwekwa ndani “Alisema DC Mwanga akisisitiza upigaji marufuku suala hilo wilayani humo.

Alisema baada ya tukio hilo jana walifanya kikao na viongozi wote wa jimbo la bumbuli ikiwemo madiwani ,viongozi wa vyama vya siasa na serikali ambapo kikao hicho kilitoa maelekezo ya serikali kupinga marufuku lambalamba.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »