SHIRIKA LA KIMATAIFA LA NGUVU ZA ATOMIKIn(IAEA) KUISAIDIA TANZANIA UZALISHAJI UMEME WA NYUKLIA

September 20, 2025 Add Comment


📌 *IAEA na Tanzania kushirikiana  kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa uzalishaji umeme wa nyuklia*


📌 *Mhandisi Mramba aishukuru IAEA kuunga mkono dhamira ya Tanzania kuwa na vyanzo endelevu, salama na vya uhakika vya nishati*



Vienna, Austria. 


Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomi (IAEA) limeeleza nia yake ya kuisaidia Tanzania katika mipango yake ya kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya Nyuklia 


Hayo yamebainika katika kikao kando ya Mkutano Mkuu wa 69 wa masuala ya Atomic uliohitimishwa tarehe 19 Septemba, 2025 nchini Austria.


Kikao hicho kilifanyika kati ya Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Prof. Carolyne Nombo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Nyuklia wa IAEA Bi Liliya Dullinet.


Kikao hicho kimekuwa sehemu ya mwendelezo wa mazungumzo ya ushirikiano kati ya Tanzania na IAEA, kikilenga kuharakisha utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kuzalisha umeme kwa kutumia nyuklia. 

Katika mazungumzo hayo, IAEA imeahidi kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika maeneo kadhaa ya kipaumbele yakiwemo Msaada wa Kiufundi na Kitaalamu kwa kusaidia Tanzania katika nyanja zote za maandalizi ya miundombinu ya nyuklia.


 Eneo lingine ni Mafunzo kwa Wataalamu wa ndani katika kujenga uwezo wa kitaalamu kwa watanzania ili kushiriki moja kwa moja katika maandalizi na uendeshaji wa miradi ya nyuklia ambapo tayari IAEA imetoa nafasi za masomo kwa Tanzania. 


Shirika hilo pia limeonesha utayari wa kuisaidia Tanzania katika kufanya Maboresho ya Mfumo wa Kisheria na Kisera kwa kutoa mwongozo katika kuimarisha sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi wa miradi ya nyuklia.


Aidha, katika hatua nyingine IAEA na Tanzania zimekubalians kuandaa kwa pamoja Mpango Kazi wa Taifa wa Utekelezaji wa Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia kuanzia hatua ya Maandalizi. 


Vilevile, Shirika hilo limeonesha utayari wa kuandaa ziara za mafunzo kwa Viongozi na wataalam wa Tanzania ili kupata uelewa na Kubadilishana uzoefu katika masuala ya teknolojia ya Nyuklia katika kuzalisha umeme. 


Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba aliwashukuru IAEA kwa utayari wao wa kuisaidia Tanzania. Pia alisisitiza kuwa dhamira ya Tanzania kuanza safari ya kuzalisha umeme wa nyuklia ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ameweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na vyanzo endelevu, salama na vya uhakika vya nishati.



Wajumbe wengine walioshiriki kikao hicho ni Mha. Joseph Kirangi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Maji na Madini kutoka Zanzibar, Mha. Athuman Kilundumya Naibu Katibu Mkuu Kilimo, Prof. Najat Mohamed,  Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Nguvu za Atomi Tanzania (TAEC), Mha Innocent Luoga, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu na Wataalam wa masuala ya Nyuklia.

MWANA FA ATAJA VIPAUMBELE VITATU ATAKAVYOTEKELEZA KATA YA KIGOMBE

September 20, 2025 Add Comment


📍Ataimarisha upatikanaji wa huduma za afya katika zahanati


📍kuhakikisha vitongoji ambavyo havina Umeme, vinapata Nishati hiyo


📍 Kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja ikiwemo upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu


📍 Leng'ese aagiza viongozi wa CCM kata, tawi na shina, kutafuta kura za wagombea wa CCM


📍 Mwenyekiti wa UVCCM wilaya Aziza awataka wana-Kigombe kuchagua wagombea wa CCM


📍 Asha na George watia Nia Ubunge Muheza, wapanda jukwaani kusaka kura za CCM


Na Mwandishi Wetu, Muheza


MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA, ametaja vipaumbele vitatu endapo wananchi wa kata ya Kigombe watamchagua katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika mji wa Kigombe, MwanaFA alisema katika mambo aliyopanga kuyatekeleza endapo atachaguliwa tena, ni kusimamia mambo ya ustawi wa jamii ya watu wa Kigombe.


"Malengo yangu niliyokuwa nayo ndugu zangu wa Kigombe endapo mtanichagua ubunge, Kwanza nitaboresha na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya katika zahanati yetu" alisema.

MwanaFA ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema atahakikisha anaiboresha zahanati ya Kigombe ili iwe na ubora wa upatikanaji wa huduma mbalimbali za afya kwa kiwango kikubwa.

Kipaumbele cha pili alichosema Zumbe wa mkoa wa Tanga, ni kuhakikisha vitongoji vitatu ambavyo havijapata Nishati ya Umeme, vitapatiwa katika mwaka ujao wa fedha.

Alisema wakati akiingia Kijiji cha Mtiti na vitongoji sita havikuwa na Umeme lakini Sasa vimebaki vitatu ambavyo navyo vitapatiwa Nishati hiyo.


Suala la tatu katika kipaumbele chake, MwanaFA alisema kuwa ataendelea kuwawezesha kiuchumi wananchi wa Kigombe ili mtu mmoja mmoja aweze kupiga hatua kiuchumi ikiwemo kuwapa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na

Halmashauri.


Aliwashukuru wananchi wa Kigombe kwa kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hatimaye katika miaka mitano iliyopita walipata kiasi cha shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya miradi ya Maendeleo.

"Ipo sababu kwanini upinzani Kigombe umekufa, zipo sababu haukufa hivi hivi, nawashukuru sana kwa kukiamini Chama Cha Mapinduzi," alisema MwanaFA.


Alisema moja ya sababu ya upinzani kufa katika kata hiyo ni historia ya kata hiyo kupata fedha nyingi za miradi ya maendeleo kuliko wakati mwingine wowote ule.


"Tumekuwa na upinzani hapa Kigombe kwasababu mambo mnayotaka yafanyike hayajafanyika...Mnataka haki mnataka mambo yenu yafanyike," alisema na kutaja miradi mbalimbali ambayo imeletewa fedha katika kipindi cha mwaka 2020-2025.

MwanaFA alisema kwa upande wa mradi wa maji jumla ya shilingi bilioni 1.3 ililetwa katika kata hiyo kwa ajili ya mradi wa maji baada ya maeneo mengi kuchimbwa visima lakini wananchi wanapata maji yenye chumvi.


Alisema wataimarisha upatikanaji wa maji katika maeneo ya Chakalaboko, Mtiti na maeneo mengine ili huduma ya majisafi na salama yaweze kupatikana katika kata hiyo.


Alisema katika sekta ya afya zahanati ya Kigombe ilipatiwa kiasi cha shilingi milioni 120 ambayo ilisaidia kupatikana nyumba ya daktari na kuboresha miundombinu ya zahanati hiyo.


"Miaka mitano ijayo tutafanya upanuzi wa zahanati yetu lakini pia uwezekano wa kupata kituo cha afya, jambo mnalotakiwa ni kufanya subra ndugu zangu," alisema.


Katika elimu ya msingi na sekondari jumla ya shilingi milioni 129.3 zililetwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule pamoja na kuweka Umeme katika shule ya sekondari.


Kuhusu uvuvi MwanaFA alisema kwamba serikali ilileta boti sita zenye thamani ya shilingi milioni 727 ambazo zimeleta nema kwa wavuvi ambao wameweza kuongeza kipato chao cha Kila siku.


Kuhusu barabara alisema kiasi cha shilingi milioni 156 kililetwa kata hiyo kwa ajili ya kukarabati  barabara ya Kigombe-Mtiti yenye urefu wa kilomita Saba ambapo iliweza kuwekewa changarawe.


Akizungumza maombi mbalimbali yaliyowasilishwa na mgombea udiwani wa kata hiyo Shahongwe Mgandi alisema Kila changamoto iliyopo katika Jimbo la Muheza ni kipaumbele chake, hivyo atazifanyia kazi.


Aliwataka wananchi wa Kigombe kumchagua kwa kura nyingi mgombea Urais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ameiheshimisha wilaya hiyo kwa kuleta miradi mingi katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wake.


"Naomba kura za kishindo kwa Dkt Samia Suluhu Hassan, tumpeni kura nyingi ili tumtie moyo ametufanyia kazi nyingi katika wilaya yetu," alisema na kuongeza,


"Nichagueni na Mimi MwanaFA Hamis Mwinjuma, lakini pia diwani wenu pamoja na kwamba yupo pekee yake lakini mnatakiwa mumpigie kura za ndiyo,".


Awali Katibu wa CCM wilaya ya Muheza Simon Leng'ese aliwataka viongozi wa CCM wa kata hiyo kuhakikisha Kamati zao za ushindi zinapita kwa wananchi kwenda kuomba kura ili chama hicho kiweze kupata kura nyingi katika uchaguzi Mkuu ujao.


Meneja kampeni wa mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo hilo, Aziza Mshakangoto na mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Muheza alisema kuwa wananchi wa Kigombe wanapaswa kujivunia kazi nzuri iliyofanywa na serikali katika kipindi kilichopita.


"Barabara hii ya Tanga Pangani ikikamilika mtaitumia kusafirisha bidhaa zenu za bahari kama mlikuwa mkisafirisha mara moja Sasa mtasafirisha mara nyingi zaidi," alisema.


Azazi alisema kuwa changamoto haziwezi kumalizwa kwa mara moja wananchi Wana hitaji kuwa wastahimilivu kwakuwa kilichofanyika pia ni hatua kubwa kwao.


George Semunga na Asha Wandi watia Nia ya ubunge katika Jimbo hilo, walipata nafasi ya kuwanadi mgombea ubunge na diwani lakini pia walimuombea kura Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwakuwa ni Rais aliyeitendea vema nafasi hiyo katika kipindi cha miaka minne na nusu.

Mwisho

KAMPUNI YA SWEDEN KUWEKEZA TEKNOLOJIA YA UMWAGILIAJI NCHINI

September 20, 2025 Add Comment

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, akijadiliana na maafisa watendaji wa kampuni ya SPOWDI, Henrik Johanson (katikati) na Christopher Thunell (kulia) katika ofisi za Ubalozi jijini Stockholm, tarehe 18 Septemba, 2025. Kampuni hiyo imekubali kuleta teknolojia ya umwagiliaji wa kilimo makini nchini Tanzania.



Balozi wa Tanzania katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, Mhe. Mobhare Matinyi, tarehe 18 Septemba, 2025, alikutana na watendaji wa kampuni ya SPOWDI, Henrik Johanson na Christopher Thunell, katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Stockholm, Sweden, kujadiliana kuhusu uwekezaji wa teknolojia ya kilimo makini cha umwagiliaji nchini.


Teknolojia hiyo ya kampuni ya SPOWDI hutumia mashine ndogo ya nishati ya jua yenye mipira ya umwagiliaji inayosambazwa shambani kutokea kwenye bwawa dogo. Umwagiliaji huu hufanyika kwa dakika 15 katika eneo la mita za mraba 500 kwa mara moja.


“Ekari moja yenye mita za mraba 4,000 inaweza kumwagilia kwa muda mfupi tu na kuokoa upotezu wa maji, muda na pia kusaidia mimea kukua kwa ubora unaostahili na hatimaye kutoa mazao mengi zaidi,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu Johanson na kuongeza kuwa matokeo yake ni kuongeza kipato na pia kulima kwa zaidi ya msimu mmoja kwa mwaka kwa gharama nafuu na bila kutegemea mvua.


Kampuni hii inakusudia kuwekeza nchini Tanzania baada ya kuvutiwa na mazingira mazuri ya Tanzania, uchapakazi wa Watanzania na sera nzuri za serikali katika uendelezaji wa sekta ya kilimo ikiwemo kusaidia upatikanaji rahisi wa mikopo kwa wakulima.


Tayari kampuni hiyo imeifikisha teknolojia hiyo katika nchi za Sweden, India, Nepal, Bangladesh, Uswizi na kwa Afrika imeanza uwekezaji nchini Kenya na hivyo Tanzania itakuwa nchi ya pili.


Balozi Matinyi aliikaribisha kampuni hiyo kufanya ziara Tanzania mwezi Novemba 2025 ili kuitambulisha teknolojia hiyo na kuanza majaribio ya awali akielezea kwamba hii itakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya serikali ya kuongeza pato la taifa, kupambana na umaskini, kuongeza ajira na uzalishaji na kuuza chakula nje ya nchi baada ya nchi kufikia usalama wa chakula kwa asilimia 140.


Stockholm

JAJI MWAMBEGELE AFANYA UKAGUZI WA VIFAA VYA UCHAGUZI MBEYA

September 20, 2025 Add Comment

 


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele Septemba 19, 2025 ametembelea  Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika Majimbo ya Uchaguzi ya Mbeya Mjini na Uyole na kupokea taarifa ya mkoa kutoka kwa wasimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kuhusu maandalizi ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025 na kisha kukagua vifaa ambavyo tayari vimepokelewa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.  Jaji Mwambegele pia alipata fursa ya kutembelea kampeni za wagombea Ubunge wa chama cha CUF na CCM katika majimbo hayo. 

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na Tume,Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu. 

"Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura"






Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza na Wasimamizi wa Uchaguzi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Mbeya ambapo alisisitiza uadilifu wakati wa utendaji kazi wao.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza na Wasimamizi wa Uchaguzi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Mbeya.
DC NYAMWESE: BIL.1.3/- KULIPA FIDIA WANANCHI MRADI WA GRIDI IMARA HANDENI

DC NYAMWESE: BIL.1.3/- KULIPA FIDIA WANANCHI MRADI WA GRIDI IMARA HANDENI

September 19, 2025 Add Comment

 

 

Na Mwandishi Wetu,Handeni

ULIPAJI fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Gridi Imara umezinduliwa rasmi katika maeneo ya Mkata, Handeni na Kilindi, huku serikali imeahidi kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha nishati bora inawanufaisha wote.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, akizindua zoezi hilo, amesema kiasi cha Sh.Bilioni 1.3 kitatumika kulipa fidia kwa wananchi hao na kueleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kuthamini utu wa mwananchi na uwekezaji alioufanya.

Amesisitiza kuwa jukumu la wananchi sasa ni kulinda miundombinu ya umeme ili manufaa ya mradi huo yaendelee kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

“Fidia hii ni kielelezo cha kujali utu na mchango wa kila mmoja. Tukiharibu au kutoheshimu miundombinu hii, hasara kubwa itakuwa yetu sote,” amesema Nyamwese.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi huo, Mhandisi Jafari Mpina, amesema serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mfumo wa umeme katika wilaya ya Handeni, hatua itakayochochea fursa za kiuchumi kwa wananchi, ikiwemo kuimarisha biashara na kuongeza ajira.

Naye, Meneja wa CRDB tawi la Handeni Carlos amebainisha kuwa malipo yote yatatolewa moja kwa moja kupitia akaunti binafsi za wanufaika, jambo linaloimarisha usalama wa fedha na kuondoa hofu ya upotevu.

Wananchi walionufaika na fidia hiyo wameishukuru serikali, wakieleza kuwa hatua hiyo imeimarisha maisha yao na kuwapa matumaini mapya ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.