PDPC YAWAASA MABLOGA KULINDA FARAGHA WAKATI WA UCHAGUZI

August 12, 2025 Add Comment

 


Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), - Innocent Mungi akitoa mada kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi.

Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, akiwasilisha mada katika mafunzo maalumu kuelekea uchaguzi mkuu mahususi kwa bloga yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Agosti 11, 2025 Jijini Dar es Salaam.

PDPC Yataka Mabloga Kulinda Taarifa Binafsi Uchaguzi 2025

Na Mwandishi Wetu.

DAR ES SALAAM, Agosti 11, 2025 – Waandishi wa habari na mabloga wametakiwa kuelimisha jamii kuhusu sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, ili kuzuia uvunjifu wa faragha na kuepusha madhara ya kisheria.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Innocent Mungy, wakati wa mafunzo maalum kuelekea Uchaguzi Mkuu, yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ombi la Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN).

Mungy alisema mabloga wana nafasi kubwa ya kuelimisha umma kuhusu sheria hiyo, hasa katika kipindi cha uchaguzi, na kuwaonya kuepuka kuchapisha taarifa binafsi za watu au wagombea.

“Ni kosa kisheria kuingilia mambo binafsi ya watu, na adhabu yake ni kali. Bloga mna wajibu wa kulinda faragha na kuepuka taarifa zinazoweza kuvunja sheria,” alisema Mungy.

Alibainisha kuwa maendeleo ya teknolojia yameongeza fursa na changamoto katika uandishi, hivyo mabloga wanapaswa kutumia majukwaa yao kwa uwajibikaji mkubwa. Pia aliahidi kuchangia mabloga ili waweze kusajili majukwaa yao kama inavyotakiwa kisheria.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Egbert Mkoko, aliwakumbusha washiriki kufuata miongozo rasmi ya uandishi wa habari za uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa blogu katika kutoa taarifa sahihi kwa jamii.

Kwa upande wake, Afisa wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Rehema Mpagama, alieleza kuwa waandishi watakaoruhusiwa kuripoti uchaguzi ni wale tu wenye ithibati, kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, aliishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa ya mafunzo hayo kupitia TCRA, akisema yatasaidia kuongeza weledi na kuimarisha usalama wa taarifa wakati wa uchaguzi.
Mhadhiri katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), Dkt. Darius Mukiza akitoa mada kuhusu Matumizi ya Mitandao ya Kijamii na Akili Unde (AI)
Afisa wa Kamati ya Bodi ya Ithibati, Rehema Mpagama, akizungumzia Maadili na Sheria kwa Waandishi wa Habari.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Egbert Mkoko, akichangia mada kuhusu Mwongozo wa Waandishi wa Habari katika Uandishi wa Habari za Uchaguzi.
Mmilikiwa Blogu ya Michuzi, Issa Michuzi akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Majadiliano yakifanyika.
Wajumbe wa Bodi ya TCRA wakijitambulisha.
Picha ya pamoja.

TBN YAKEMEA VIKALI MANABII WA MITANDAONI,YATAKA WAWAJIBIKE KWA SHERIA

August 11, 2025 Add Comment

Mtandao wa Bloga Tanzania (TBN) umekemea vikali tabia inayoshamiri ya watu kujinadi kufanya utabiri kwa watu na taifa kupitia mitandao ya kijamii, ukisema vitendo hivyo vinakiuka Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.


Kauli hiyo imetolewa kama azimio katika kikao kazi cha mafunzo ya mabloga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.


Mabloga hao wameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kushirikiana kuwasaka na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaohusika na vitendo hivyo.


Katika kikao hicho, mabloga walibainisha kuwa kumeibuka kundi la watu wanaodai kuwa ni manabii na kutoa kauli zinazokiuka sheria za nchi na kuleta taharuki kuelekea uchaguzi. Walisisitiza kuwa baada ya kuchambua Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Act), walibaini kwamba 'utabiri' wa namna hiyo unavuruga haki ya msingi ya faragha ya wahusika.


Kwa mujibu wa Bw. Innocent Mungy, mtoa mada kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), sheria hiyo inakataza mtu kuzungumziwa kuhusu afya yake, mwenendo, au taarifa zake binafsi kutolewa bila ridhaa yake. Mungy alisisitiza kuwa sheria hii ina adhabu kali na lazima ifuatwe na kila mtu, si tu mabloga na waandishi wa habari.


Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na TCRA, yalilenga kuwaandaa mabloga kuripoti habari za uchaguzi kwa weledi na uadilifu. 


Pamoja na mada ya ulinzi wa taarifa binafsi, mada nyingine muhimu zilizotolewa ni pamoja na Mwongozo wa Waandishi wa Habari katika Uchaguzi na Matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika uandishi wa habari.


Lengo kuu la mafunzo haya ni kuongeza uwezo wa mabloga kuhakikisha wanafuata sheria na maadili ya uandishi, jambo linalotazamiwa kuchangia mazingira ya uchaguzi yenye amani na utulivu.


@@@@@@@@@@@@@

DKT.BITEKO ASHIRIKI MAZISHI YA SPIKA MSTAAFU NDUGAI

August 11, 2025 Add Comment




Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Agosti 11, 2025 ameshiriki mazishi ya Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Job Yustino Ndugai yaliyofanyika katika Kijiji cha Sujulile, wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma.

Mazishi hayo yameongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama Cha Mapinduzi pamoja na Viongozi wa Dini.

REA YAZIDI KUHAMASISHA NISHATI SAFI, YATOA BILIONI 4.37KWA JESHI LA KUJENGA TAIFA

August 11, 2025 Add Comment


*📌JKT yaipongeza REA utekelezaji wa miradi ya nishati safi*


*📌REA yaiwezesha JKT asilimia 76 ya miradi ya nishati safi*


*📌Watumishi 7,000 wa JKT kupatiwa Mtungi wa kilo 15 wa LPG pamoja na Jiko lake la sahani mbili kila mmoja*


📍Makutupora - Dodoma


Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024 – 2034).

Hayo yamebainishwa leo Agosti 11, 2025 na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Kanali Juma Mrai wakati akifungua mafunzo kwa washiriki toka vikosi  22 vinavyonufaika na mpango wa nishati safi JKT katika bwalo la vijana 834KJ (Makutupora) jijini Dodoma

"Hii yote ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 zihame kutoka katika matumizi ya nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia, " Ameongeza Kanali Mrai.

Aidha, ameipongeza REA kwa kuhamasisha na kuwezesha  matumizi ya nishati safi ili kutunza mazingira na kuepuka athari za kiafya zinazohusiana na utegemezi mkubwa wa nishati isiyo kuwa safi

"REA imeiwezesha JKT kwa asilimia 76 Sawa na Shilingi Bilioni 4.37 ya utekelezaji wa nishati safi katika kambi 22 za JKT kwa kuzipatia mashine za kutengeneza mkaa  Mbadala 60, majiko  banifu 291, mifumo ya gesi ya LPG 180 na masufuria yake, Mkaa Mbadala tani 220, mafunzo kwa vijana 50,000 pamoja na mifumo ya Gesi Vunde 9 " Amesisitiza Kanali Mrai. 

Katika hatua nyingine, amewataka watendaji waliolengwa kutumia mashine za kutengeneza mkaa mbadala, majiko banifu na majiko ya gesi pamoja na mkaa rafiki wa mazingira unaotokana na mabaki ya mazao ya shambani kupatiwa elimu ili kuwa na uwezo wa kubaini na kutatua changamoto za nishati hiyo na hatimaye bidhaa hizo kuleta tija kwa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mha. Advera Mwijage amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo maafisa na askari wa vikosi vilivyopo katika mpango wa REA ili waweze kuwa mabalozi  wazuri wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye maeneo yao ya kazi.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatachangia katika mlolongo mzima wa kuwa na matumizi endelevu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa sababu mafunzo haya yanatoa fursa ya kupata ujuzi utaowawezesha Kusimamia mifumo ya Nishati safi vizuri.

Aidha Amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa kwa utekelezaji mzuri wa mradi na kuahidi ushirikiano katika kuhakikisha tunakamilisha mradi huu kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mha. Mwijage amebainisha kuwa, tayari REA imeidhinisha zaidi ya milioni 800 kwa ajili ya watumishi 7,000 wa JKT kupatiwa Mtungi wa kilo 15 wa LPG pamoja na Jiko lake la sahani mbili kila mmoja  ikiwa ni sehemu wa kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya Kupikia kwa mtu mmoja mmoja.



WAZIRI MKUU AMWAKILISHA DKT SAMIA MAZISHI YA HAYATI NDUGAI

August 11, 2025 Add Comment


*_Asema aliimarisha ushirikiano kati ya Bunge na Serikali_*

*_Atoa rai kwa Watanzania kuenzi mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake_*

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Agosti 11, 2025 amemwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Job Yustino Ndugai, yaliyofanyika shambani kwake, kijiji cha Msunjulile, wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Akizungumza katika ibada ya mazishi, Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuenzi mema yote yaliyofanywa na Hayati Ndugai enzi za uhai wake, akisema mchango wake katika uongozi wa Bunge na Taifa kwa ujumla utabaki kuwa kumbukumbu muhimu kwa vizazi vijavyo.

Amesema kuwa akiwa mwakilishi wa wananchi wa Kongwa, hayati Ndugai ametoa mchango mkubwa katika kipindi cha miaka 20 ya utumishi wake, na kwamba wote ni mashuhuda wa maendeleo makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali za maendeleo pamoja na huduma za kijamii. “Serikali itaendelea kumuenzi kwa yale yote aliyoyafanya kwa wanaKongwa”

Aidha, Waziri Mkuu ameeleza kuwa hayati Ndugai alikuwa mlinzi wa taratibu za Bunge na mshirika wa karibu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Bunge na Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa, akisisitiza mawasiliano ya uwazi, mshikamano na mwelekeo wa pamoja wa utekelezaji wa ajenda za kitaifa.

Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa amemtaja hayati Ndugai kama kiongozi mwenye weledi, uadilifu, unyenyekevu, na mchapakazi ambaye alibeba heshima ya mkoa wa Dodoma na jimbo la Kongwa kupitia uongozi na siasa za uwajibikaji.

Pia, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itasimamia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ya kukamilishwa kwa masuala yote yaliyoanzishwa na Hayati Ndugai, pamoja na kuendeleza makumbusho ya Kongwa ikiwa ni kielelezo cha kupigania uhuru kwa nchi za kusini mwa afrika. “Tutasimamia agizo hili kwa ukamilifu.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Kongwa na Watanzania wote kwa ujumla  kutokana na msiba wa hayati Ndugai.

Naye, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa wanaamini katika kumuenzi hayati Ndugai na watamkumbuka daima kwa kuendeleza misingi pamoja na mambo mema yote aliyoyatenda wakati wa uhai wake.



Mazishi ya Hayati Ndugai yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Zena Saidi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongela, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, viongozi wengine kitaifa, ndugu, jamaa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.

Hayati Job Ndugai alifariki agosti 06, 2025 jijini Dodoma kwa Shinikizo la damu lililoshuka sana