Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

UWEKAJI WAZI DAFTARI NA UBORESHAJI AWAMU YA PILI

May 01, 2025 Add Comment

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akitembelea na kukagua vituo vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili mkoani Njombe linalokwenda sambamba na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura ambapo mikoa 15 imeanza zoezi hilo litafanyika kwa siku saba kuanzia Mei 1 hadi 7, 2025. (Picha na INEC).

Wananchi wa Kata ya Kihesa katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mkoani Iringa wakikagua majina yao katika daftari la awali la wapiga Kura lililobandikwa katika kiuo cha kujiandikishia wapiga Kura kilichopo ofisi ya Mtendaji Kihesa. Tume Huru ya taifa ya Uchaguzi imeanza awamu ya pili ya Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura katika mikoa 15 ya Tanzania bara kuanzia Mei Mosi hadi 07, 2025 unaokwenda sambamba na uwekaji wazi wa daftari la awali. (Picha na INEC). 



 

MWANASHERIA CHIPAMBA: KUJENGA JENGO BILA MIUNDOMBINU YA WALEMAVU FAINI NI MILIONI 20

April 30, 2025 Add Comment

 

Mwanasheria Baraka Chipamba wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT),  akizungumza na watu wenye ulemavu kutoka Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB), Mkoa wa Dar es Salaam alipokuwa  akitoa elimu kuhusu sheria ya watu wenye ulemavu Aprili 29, 2025.

.............................

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MWANASHERIA Baraka Chipamba wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT)  amesema ni kosa kisheria kujenga jengo ambalo halina miundombinu ya kuwasaidia watu wenye ulemavu na faini yake ni Sh. Milioni 20.

Chipamba aliyasema hayo Aprili 29, 2025 wakati akizungumza na watu wenye ulemavu kutoka Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB), Mkoa wa Dar es Salaam alipokuwa  akitoa elimu kuhusu sheria ya watu wenye ulemavu mafunzo yaliyoratibiwa na LRCT na kufanyika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

 Alisema kosa hilo la kujenga jengo bila ya kuwa na miundombinu ya watu wenye ulemavu likifanywa na Serikali faini yake ni Sh. Milioni 2 na isizidi Milioni 20 na kama litafanywa na mtu binafsi ni faini isiyopungua Sh. 500,000 hadi Sh.Milioni 7 au kifungo cha mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya watu wenye ulemavu kama  wananchi wengine wanayo haki ya kuheshimiwa, kutobaguliwa, kupata ajira, matunzo na stahiki zote wanazozipata watu wengine ikiwemo elimu. 

“ Upo umuhimu wa kuwepo vyama vya watu wenye ulemavu ili kuwakilisha na kujisemea katika ngazi mbalimbali, kufanya utambuzi wa mahitaji yao pia kutathmini huduma zinazotolewa na kuchochea maendeleo yao,” alisema Chipamba.

Alisema Serikali ya Tanzania imeridhia au kuonesha nia ya kuwa sehemu ya juhudi za kimataifa ya kuwainua na kuwalinda watu wenye ulemavu kwa kuwapatia fursa mbalimbali.

“Tunatambua Tanzania imeridhia na kusaini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD-2006 na Mkataba wa Nyongeza wa Haki za Watu Wenye Ulemavu 2009). Lakini pia tunatambua kuwa kuna mambo mengi yamekwisha tekelezwa na Serikali,” alisema Chipamba.

Mwanasheria wa Tume hiyo, Vicky Mbunde ambaye alitoa elimu ya jinsi ya kuandika wosia na kufungua shauri la mirathi alisema Watu wenye ulemavu wanayo haki na nafasi ya kujiendeleza na kupata huduma katika jamii sawa na watu wasio na ulemavu.

Alisema ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maisha ya kila siku katika jamii hauna budi kulenga katika kupunguza au kuondoa maisha ya utegemezi hivyo aliwahimiza kufanya kazi kwa bidi kama vile ujasiriamali na shughuli zingine ili kujiletea maendeleo yao badala ya kusubiri kusaidiwa.

Katika mafunzo hayo mambo kadhaa yaliibuka ikiwa ni pamoja na jinsi wanavyoitwa ni ‘Watu wenye Ulemavu au Walemavu’ ambao wanasheria wa Tume hiyo walieleza kuwa wanatambulika kama ni Watu Wenye Ulemavu na siyo Walemavu.

Akichangia mada kuhusu suala la kuandika wosia na mgawanyo wa mali zilizoachwa na marehemu kwa wanufaika baada ya kufungua mirathi, Azamu Mohamed kutoka Yombo Dovya alisema dini ya Kiislam haimtambui mtoto aliyezaliwa kwa mama mwingine nje ya ndoa jambo ambalo linawafanya wanaume wengi kuwakataa watoto hao hivyo kushindwa kupata mgao wa mali za baba zao pindi wanapofariki.

“Wanaume ule ujasiri mliotumia wa kutoka kwa wake zenu na kwenda kuchepuka na kuwapata watoto hao mnatakiwa kuuonesha kwa kuwatambulisha kwa wake zenu na ndugu ili nao wajulikane na kupata mgao huo badala ya kuwakana,” alisema.

Mweka hazina wa Jumuiya hiyo, Seif Jega, akizungumza baada ya kupata nafasi ya kushukuru kwa niaba ya washiriki baada ya mafunzo hayo aliupongeza uongozi wa Tume hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo kwa watu wenye ulemavu na kuomba yawe endelevu ikiwa ni pamoja na kuyafikisha vijijini wenzao na jamii waweze kuielewa jambo ambalo litaweza kupunguza unyanyapaa kwa kundi hilo.

Kuhusu Tume hiyo, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) ni Idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Sura ya 171, na ilianza kazi rasmi tarehe 21 Oktoba, 1983. 

Kwa mujibu wa sheria, Tume ina jukumu la kufanya mapitio ya sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ziandane na mazingira ya wakati uliopo kwa maendeleo endelevu.          

Mwanasheria Vicky Mbunde wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT), akitoa elimu kuhusu namna ya kuandika Wosia pamoja na kufungua mirathi.
Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Iddi Damka, akiongoza mafunzo hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Judika Magezi akizungumza.
Mafunzo yakiendelea.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Maswali yakiulizwa kutoka kwa washiriki wa mafunzo hao.
Asha Kinyama akichangia jambo kwenye mafunzo hayo
Maswali yakiendelea kuulizwa.
Margareth Mhina, akizungumzia umuhimu wa faragha wakati wa kumuhudumia mtu mwenye ulemavu anapokwenda kupata matibabu hospitalini.
Maswali zaidi yakiulizwa.
Taswira ya mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea. 

WAZIRI MAVUNDE ATOA MAAGIZO MATANO KWA MENEJIMENTI YA TUME YA MADINI

April 30, 2025 Add Comment


▪️Asisitiza kuzingatiwa kwa sheria ya Madini


▪️Ataka ofisi za Madini kusimamia haki katika usuluhishi wa migogoro


▪️Maafisa Madini watakiwa kuongeza ubunifu katika utekelezaji majukumu


▪️Makusanyo ya maduhuli yafikia asilimia 86.53_


▪️Apongeza utulivu Sekta ya Madini

 

WAZIRI wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde (MB) ametoa maelekezo matano kwa Menejimenti ya  Tume ya Madini hasa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuzingatia na kusimamia  sheria katika utekelezaji wa majukumu yao na kufikiri nje ya boksi ili kuwa na kitu cha ziada katika kuendeleza Sekta ya Madini.

 


Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Aprili 30, 2025 jijini Dodoma kwenye ufunguzi wa kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini ambapo  amewataka watendaji kuwa wabunifu katika maeneo yao, washirikiane, mkoa mmoja na mkoa mwingine pamoja na kushauriana.

 

“Kwenye Sekta ya Madini  ukiweka sheria pembeni utaivuruga sekta,  kuna wakati matumizi ya busara huwa yanahitajika lakini sheria kwanza, kaisimamieni, kesho keshokutwa mtu atakuuliza jambo lingine lolote dhamira yako ilikuwa nini na sheria inasema nini, kasimamie sheria kwanza na kama kuna maelekezo tofauti yasitokane na wewe, wewe katimize  wajibu wako wa kusimamia sheria ni muhimu sana,”amesema Waziri Mavunde.

 


Agizo la pili ambalo amelitoa Mheshimiwa Mavunde ni kutaka ubunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

 

“Nataka mkawe wabunifu, tumenunua magari 101 mengine yanakuja pikipiki 140  Rais Daktari Samia Suluhu Hassan ametupatia nyenzo, nataka mfikiri nje ya boksi  nini ufanye kwenye eneo lako ili sekta  iweze kushamiri zaidi, isiwe ‘business as usual’ tunatamani kuona kila mtu katika eneo lake anajitahidi,”amesema.

 


Katika  hatua nyingine Mheshimiwa Mavunde amewapongeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kutorudi nyuma  na kuhakikisha kila mmoja anavuka lengo alilopangiwa na kuongeza kuwa,

 


“Mjitahidi kutafuta njia za kuongeza makusanyo pasipo kuleta athari kwa watu mnaowasimamia. Zipo njia nyingi za kufanya simamieni hilo, sisi tunaingiza fedha nyingi sana katika mfuko mkuu wa Serikali, miradi inayokuja mikubwa naamini tutafanya vizuri zaidi.

 


Katika agizo la nne la uadilifu Waziri Mavunde ameeleza kuwa hivi karibuni Sekta ya Madini imekuwa na utulivu pasipo kuwepo na malalamiko yoyote na kuwataka Maafisa  Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kutenda haki pasipo kuonea wadau wa madini na kutatua migororo na changamoto zinazowakumba wadau wa madini.

 

Amewasisitiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanatatua migogoro kwa kufuata haki ili kujenga imani na wachimbaji wa  madini na kuendelea kutoa elimu kuhusu Sheria na Kanuni za  Madini ili kupunguza migogoro kabisa.

 


Akitoa agizo la Tano Mheshimiwa Mavunde amesema kuwa ili kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini, imeundwa kamati maalum ya kuwajengea uwezo watanzania kushiriki kikamilifu katika Sekta ya Madini ili baadaye wawe wachimbaji wakubwa wa madini na kuelekeza Watendaji wa Tume ya Madini kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo.

 


“Wanapokuwepo wachimbaji wakubwa ambao ni wazawa faida lukuki zinapatikana ikiwa ni pamoja na ajira, mapato na ongezeko la manunuzi ya bidhaa na huduma za ndani ya nchi,” amesema  Waziri Mavunde.

 

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani madini nchini ambapo mpaka sasa wawekezaji wengi wamejitokeza kwenye ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani katika mikoa ya kimadini ya Chunya, Dodoma, Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Rukwa na Lindi.

 

Amesema kutokana na utendaji mzuri wa Sekta ya Madini hasa mchango wake kwenye Pato la Taifa kufikia asilimia 10.1 nchi ya Kenya kupitia Waziri wa Madini na Uchumi wa Bluu, Mheshimiwa Ali Hassan Joho wameomba kuja kujifunza nchini Tanzania.

 

Aidha, amewataka wachimbaji wa madini waliopewa leseni kuzifanyia kazi na kwa ambao hawajazifanyia kazi hatua mbalimbali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuandikiwa hati za makosa na kufutwa kwa mujibu wa sheria.

 

 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba akizungumza katika mkutano huo amewataka Viongozi wa Tume ya Madini kuendelea kuimarisha upendo sambamba na kushirikiana ili Sekta ya Madini iendelee kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.

 

Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha akielezea hali ya makusanyo ya maduhuli katika Tume ya Madini amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 753.8 sawa na asilimia 85.45 ya lengo kilikusanywa.

 

Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 kuanzia mwezi Julai hadi Aprili 29, 2025 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bulioni 862.64 ambacho ni sawa na asilimia 86.53 ya lengo la Shilingi Trilioni Moja.

 

“Tunaamini kiasi kilichobaki tutakikamilisha ifikapo Juni, 30 mwaka huu kwa kuongeza nguvu na ubunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli na udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato,” amesisitiza Kamishna Mwasha.

RAIS MHE DKT SAMIA SULUHU AONGOZA KIKAO CHA BARAZA LA MAWAZIRI IKULU CHAMWINO MKOANI DODOMA

April 29, 2025 Add Comment

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 29 Aprili, 2025. 


WATANZANIA WATAKIWA KUENZI MUUNGANO

April 29, 2025 Add Comment



Na Paskal Mbunga, Tanga.


WATANZANIA wametakiwa kuuenzi Muungano wa Tanzania kwa sababu ni tunu kubwa tuliyoachiwa na wazee wetu waasisi wa Muungano huo. hayati Mwalimu Julius Nyerere na hayati Mzee Amri Abeid Karume wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

AÄ·izungumza na hadhara ya wakazi wa Jiji la Tanga Jumamosi hii ya kuadhimisha mwaka wa 61 wa kuzaliwa mwungano huo , Spika wa Bunge la Baraza la Mapinduzi Zanzibar,  Zubeir Maulid, alisema kwamba mapinduzi hayo yameleta mafanikio makubwa.

Alitaja mafanikio yaliyoletwa na Muungano huo ni pamoja na uwepo wa Rais Samia Hassan madarakani kwani bila Muungano, Mheshimiwa Samia asingeipata nafasi hiyo kutokana na kigezo cha uraia wake wa Zanzibar.

Alisema kwamba kuungana kwa nchi hizo mbili kumeimarisha ulinzi na usalama katika mipaka yetu ikiwa ni pamoja na ya baharini na nchi kavu.

Akisisitiza umuhimu wa Muungano huo kwa Watanzania, Spika Zubeir alisema uchumi wa nchi mbili hizi umepaa kutokana na kuongezeka kwa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Kiongozi huyo kutoka Zanzibar aliwachekesha wananchi waliohudhuria hafla hiyo pale aliposema kwamba matunda ya Muungano ni mengi.   

"Sasa hivi ndoa zimeongezeka sana kati ya  watu wanaooana kutoka Zanzibar na wale kutoka Tanzania Bara".

Hata hivyo, Mheshimiwa Maulid aliwahimiza Watanzania kudumisha amani na kuhakikisha kuwa kila mwenye sifa ya kupiga kùra anahakikisha anatumia haki yake hiyo ifikapo mwezi Oktoba, 2025.

Awali akimkaribisha Mgeni huyo rasmi,  Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani alisema kuwa Mkoa wa Tanga uko mbele katika kuitikia wito wa kujiandikisha kupiga kura kwani hadi sasa  Mkoa wa Tanga unaongoza kitaifa kwa kuandisha katika daftari la wapiga kura ambapo hadi sasa waliojiandisha ni karibu asilimia mia moja na sitini.

Naye Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huu, Mhe. Rajabu Abrahamani alimhakikishia Spika Zubeir kwamba kwa mapenzi makubwa waliyomwonyesha Rais Samia wakati wa ziara yake iliyofana sana mkoani hapa mwezi uliopita, ana uhakika kwamba Mkoa huu utaongoza katika kura za kumpigia Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu ujao, Oktoba, 2025.

(MWISHO)