WAZIRI DKT HOMERA AZINDUA MIFUMO ITAKAYOWEZESHA WANANCHI KUPATA HUDUMA ZA UMEME KWA HARAKA NA URAHISI

October 06, 2026




📌Aipongeza TANESCO kwa kutekeleza maono ya Rais. Dkt. Samia  ya kutumia ubunifu katika kuhudumia wananchi.



Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amezindua mifumo mipya ya kuhudumia wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Mkataba wa Huduma kwa Wateja ulioboreshwa, ikiwa ni hatua inayolenga kuhakikisha wateja wakubwa na wadogo wa Shirika hilo wanapata huduma kwa haraka na urahisi.


Akizindua mifumo hiyo jijini Dar es Salaam tarehe 6 Oktoba 2026, Dkt. Homera amesema TANESCO imeonesha dhamira ya kupiga hatua zaidi katika kuboresha huduma kwa wateja, akieleza kuwa hatua hiyo ina umuhimu mkubwa katika maslahi ya Taifa, hususan katika utekelezaji wa Dira 2050 na maono ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha taasisi zinatumia ubunifu na teknolojia katika kuboresha huduma kwa wananchi.

Mifumo aliyoizindua ni pamoja na 'Twiga Assistant' suluhisho la kisasa linalotumia akili mnemba (AI) na kumwezesha mteja kupata huduma saa 24 kwa siku bila kulazimika kupiga simu TANESCO na  'Twiga Premium Portal' jukwaa maalum la kidijitali litakalowawezesha wateja wakubwa kupata huduma mbalimbali kwa urahisi zaidi.

Aidha, Dkt. Homera amezindua namba maalum 185 kwa ajili ya wateja wakubwa, itakayowawezesha kupata huduma za haraka, za moja kwa moja na zenye kipaumbele pamoja na uzinduzi wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Wakubwa ili kuhakikisha kundi hilo linapata huduma zinazokidhi mahitaji yake.

Pamoja na kuipongeza TANESCO kwa ubunifu huo uliofanywa na wataalamu wa ndani, Dkt. Homera amelitaka Shirika hilo kuhakikisha Mkataba wa Huduma kwa Wateja unatekelezwa kwa vitendo katika ngazi zote na ahadi zilizomo ndani yake zinakuwa sehemu ya utamaduni wa kazi wa kila mtumishi. Pia, amesisitiza mifumo yote iliyozinduliwa ifanye kazi kwa ufanisi muda wote na itumike kwa vitendo ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Vilevile, ameelekeza TANESCO kutoa elimu ya kutosha kwa makundi yote ya wateja kuhusu mifumo hiyo na namna ya kuitumia kupata huduma na kutatua changamoto mbalimbali. 

Ameitaka pia TANESCO kuongeza matumizi ya takwimu na maoni ya wateja katika kufanya maamuzi, huku kila lalamiko la mteja likitumika kama fursa ya kuboresha huduma.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kulinda taarifa za wateja na mifumo ya kidijitali kwa kuzingatia sheria na viwango vya usalama wa taarifa, sambamba na kukiwezesha kikamilifu Kitengo cha Huduma kwa Wateja Wakubwa kutoa huduma bora na kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika Sekta ya Nishati umeendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, ambapo uwezo wa kuzalisha umeme umefikia MW 4,606, sawa na ongezeko la asilimia 21.32, huku mahitaji ya juu ya umeme yakifikia MW 2,316, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.97 ikilinganishwa na mwaka 2025.

Amesema ongezeko hilo la mahitaji ya umeme linaenda sambamba na kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaohitaji kuhudumiwa, hivyo mifumo hiyo mipya itachangia utekelezaji wa malengo ya Serikali, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotambua nishati kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi.

Katika hafla hiyo, Dkt. Homera amesisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inafikia uwezo wa kuzalisha megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 akieleza kuwa lengo hilo linawezekana kutokana na Wizara na taasisi zake, ikiwemo TANESCO, kuwa na wataalamu wanaofanya kazi kwa weledi, sambamba na kuendelea kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, ukiwemo Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu ambao awamu yake ya pili inahusisha  MW 100

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amesema huduma zilizozinduliwa, zikiwemo Twiga AI Chatbot, Twiga Premium Customer Portal, Premium Customers Toll Free Line, Premium Customer Service Section  pamoja na Mkataba wa Huduma kwa Wateja ulioboreshwa, zinaendana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa pamoja na kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini, huduma zinazotolewa kwa wananchi zinaendelea kuboreshwa kupitia teknolojia, ubunifu na mifumo ya kisasa.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »