NCHI 18 ZAKUSANYIKA ARUSHA KUJENGA UWEZO WA USALAMA WA NYUKLIA

October 06, 2026


Na Mwandishi Wetu - ARUSHA.


Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika juhudi za kikanda na kimataifa za usalama wa nyuklia baada ya kukutanisha wataalamu na washiriki kutoka nchi 18 katika warsha ya kikanda inayolenga kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika masuala ya usalama wa nyuklia.

Warsha hiyo ya siku tano, inayofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA), ikiwa na lengo la kujadili namna Vituo vya Usaidizi wa Usalama wa Nyuklia (Nuclear Security Support Centres – NSSCs) vinavyoweza kusaidia nchi kujenga na kudumisha wataalamu wenye uwezo wa kusimamia masuala ya usalama wa nyuklia.

Akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), ambaye pia ni Mratibu wa Kitaifa wa Tanzania na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA) (National Liaison Officer – NLO), Prof. Najat Kassim Mohamed, amesema matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani yanahitaji kwenda sambamba na uwepo wa wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kuhakikisha nyenzo za nyuklia na vyanzo vingine vya mionzi vinatumika kwa uwajibikaji na kulindwa ipasavyo.

Amesema mifumo bora na vifaa vya kisasa pekee haviwezi kuhakikisha usalama wa nyuklia bila kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kuvitumia, kuvitunza na kuchukua hatua stahiki pale linapotokea tukio linalohusisha usalama wa nyuklia.

“Maendeleo ya rasilimali watu ni jukumu endelevu la kila nchi. Tunahitaji kutambua ujuzi unaohitajika, kujua uwezo tulionao, kutoa elimu na mafunzo yanayofaa na kutathmini kama mafunzo hayo yameleta matokeo yanayotarajiwa,” amesema Prof. Najat.

Warsha hiyo imekusanya watu 48 kutoka nchi 18, wakiwemo washiriki 25 wanaohudhuria moja kwa moja jijini Arusha, washiriki 18 wanaoshiriki kwa njia ya mtandao pamoja na wataalamu watano. Wataalamu wanaowezesha warsha hiyo wanatoka Algeria, Misri, Malaysia na Tanzania.

Prof. Najat amesema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya pamoja ya nchi zinazoshiriki katika kujenga uwezo endelevu wa kukabiliana na changamoto za usalama wa nyuklia, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya kuhifadhi maarifa na kuendeleza utaalamu hata pale watumishi wanapobadilisha majukumu au kuondoka katika utumishi.

Kwa mujibu wa Prof. Najat, Vituo vya Usaidizi wa Usalama wa Nyuklia vina nafasi muhimu katika maeneo matatu yanayokamilishana, ambayo ni maendeleo ya rasilimali watu, msaada wa kiufundi na msaada wa kisayansi. Maeneo hayo yanasaidia nchi kuwa na wataalamu wenye uwezo, vifaa na mifumo inayofanya kazi kwa ufanisi pamoja na utaalamu wa kisayansi unaohitajika katika kushughulikia masuala ya usalama wa nyuklia.

Katika kipindi cha warsha hiyo, washiriki watajadili misingi ya mifumo ya usalama wa nyuklia na namna ya kuifanya iwe endelevu, nafasi ya Vituo vya Usaidizi wa Usalama wa Nyuklia katika maendeleo ya rasilimali watu, pamoja na umuhimu wa kuwa na mipango ya kitaifa ya kujenga uwezo wa wataalamu wanaohusika na usalama wa nyuklia.

Majadiliano pia yataangalia kwa kina maeneo matatu muhimu ya usalama wa nyuklia ambayo ni kuzuia matukio ya kiusalama, kugundua vitendo au matukio yanayoweza kuhatarisha usalama na kuwa na uwezo wa kuchukua hatua stahiki yanapotokea.

Mada nyingine zitakazojadiliwa ni pamoja na usimamizi na utunzaji wa maarifa ndani ya taasisi, kubaini mapungufu katika uwezo uliopo, kujenga uwezo wa kitaifa na namna ya kutekeleza mipango ya maendeleo ya rasilimali watu kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kila nchi.

Prof. Najat amewataka washiriki kutumia warsha hiyo kubadilishana uzoefu kwa uwazi, ikiwemo kueleza mafanikio, changamoto, upungufu wa rasilimali na vikwazo wanavyokutana navyo katika nchi zao ili majadiliano hayo yasaidie kupata njia zinazoweza kutekelezeka katika mazingira halisi.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya warsha hiyo hayatapimwa kwa idadi ya mada zitakazowasilishwa pekee, bali kwa namna maarifa na uzoefu watakaoupata washiriki vitakavyosaidia kuleta maboresho katika taasisi na nchi zao baada ya kumalizika kwa warsha.

Warsha hiyo pia inatoa fursa kwa nchi zinazoshiriki kujifunza kutokana na uzoefu wa kila mmoja, kubaini mbinu zinazoweza kutumika katika mazingira tofauti na kuimarisha mahusiano ya kitaalamu yatakayosaidia kuendeleza ushirikiano katika masuala ya usalama wa nyuklia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TAEC, Bwana Peter Ngamilo, amesema kufanyika kwa warsha hiyo nchini Tanzania ni fursa muhimu ya kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa usalama wa nyuklia na kuonesha mchango wa ushirikiano wa kimataifa katika kujenga uwezo wa wataalamu wanaosimamia eneo hilo.

“Usalama wa nyuklia ni suala linalohitaji ushirikiano, ujuzi na uelewa wa pamoja. Kukutana kwa wataalamu kutoka nchi 18 hapa Arusha kunatoa nafasi ya kubadilishana uzoefu na maarifa ambayo yatasaidia kuimarisha uwezo wa nchi zetu katika kulinda nyenzo za nyuklia na vyanzo vingine vya mionzi,” amesema Ngamilo.

Ngamilo amesema TAEC itaendelea kutoa elimu na taarifa sahihi kwa umma kuhusu masuala ya usalama wa mionzi na nyuklia ili wananchi wawe na uelewa mpana kuhusu matumizi salama na yenye manufaa ya teknolojia ya nyuklia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akihitimisha hotuba yake, Prof. Najat ameishukuru IAEA kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kujenga uwezo wa kitaifa na kikanda katika usalama wa nyuklia, huku akiwataka washiriki kutumia kikamilifu siku tano za warsha hiyo kupata maarifa na uzoefu utakaosaidia kuleta maboresho katika nchi na taasisi wanazowakilisha.

Warsha hiyo inatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 9, 2026, jijini Arusha.









Share this

Related Posts

Previous
Next Post »