MIJADALA YA CATA KUWA CHACHU YA KUBORESHA ZAIDI HUDUMA ZA KODI TANZANIA – CG MWENDA

October 07, 2026

 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema mijadala ya Mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola CATA, itakuwa chachu ya kuboresha zaidi huduma za kodi nchini. Ameyasema hayo leo, tarehe 7 Oktoba 2026, wakati akiongoza ujumbe wa CATA katika ziara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya programu ya mkutano huo unaofanyika tarehe 5–9 Oktoba 2026.

Amesema ziara hiyo imewapa Wakuu wa Mamlaka za Mapato na Makamishna kutoka nchi mbalimbali fursa ya kujifunza uzoefu wa EAC katika matumizi ya teknolojia, ubadilishanaji wa taarifa na uboreshaji wa mifumo ya Forodha, hatua zinazochangia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kurahisisha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Stephen Mbundi, ameipongeza TRA kwa maandalizi mazuri ya Mkutano wa 46 wa CATA, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Amesema matumizi ya teknolojia, ubadilishanaji wa taarifa na uunganishaji wa mifumo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa Mamlaka za Mapato.

Katika ziara hiyo, wajumbe walipata fursa ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa Single Customs Territory na namna EAC inavyowezesha ushirikiano wa Forodha miongoni mwa Nchi Wanachama. Ziara hiyo pia imewapa wajumbe nafasi ya kubadilishana uzoefu kuhusu mageuzi ya kidijitali na changamoto zinazokabili Mamlaka za Mapato katika ukanda huo.

Rais wa CATA amesema matumizi ya teknolojia na ubunifu ni chachu ya kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa walipakodi. Amesema ujumbe huo umejikita katika kujifunza matumizi ya mifumo ya kidijitali na namna teknolojia inavyoweza kurahisisha michakato ya kodi na huduma kwa walipakodi.

Aidha, ameipongeza Tanzania kupitia TRA kwa kuendelea kuboresha mifumo rafiki kwa walipakodi na kuweka mazingira yanayorahisisha ulipaji wa kodi. Amesisitiza kuwa Mamlaka za Mapato barani Afrika zinapaswa kuendelea kujiboresha katika matumizi ya teknolojia na ubunifu ili kuongeza ufanisi wa ulipaji na ukusanyaji wa mapato.

Akihitimisha, Bw. Mwenda amesema TRA itaendelea kutumia maarifa na uzoefu unaopatikana kupitia mijadala ya CATA katika kuboresha huduma kwa walipakodi, kurahisisha ulipaji wa kodi na kuimarisha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Taifa. Mkutano wa CATA 46 unaendelea jijini Arusha ukiwa na kaulimbiu, “Leveraging Technology for Efficient Revenue Collection.”









Share this

Related Posts

Previous
Next Post »