WAZIRI KIKWETE: SOMALIA IMEKUJA KUJIFUNZA MAFANIKIO YA MATUMIZI YA MIFUMO YA KIDIJITARI KATIKA UTUMISHI WA UMMA NCHINI TANZANIA

August 27, 2026


Na Lusungu Helela, Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhwani Kikwete, amesema uamuzi wa Serikali ya Somalia kumtuma Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma nchini Tanzania ni ishara ya kutambua mafanikio yaliyofikiwa na Tanzania katika eneo la matumizi ya mifumo katika masuala ya Utumishi wa Umma nchini.

Mhe. Kikwete amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na ujumbe wa Serikali ya Somalia unaoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Utumishi wa Umma, Hirsi Jama Ganni, uliofika nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Amesema ujio wa ujumbe huo unaonyesha kuwa Somalia inatambua na kuthamini uzoefu wa Tanzania katika uendeshaji wa Serikali, utumishi wa umma na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Ukiona wenzako wanakufuata hasa katika eneo hili ambalo sisi ni watoa huduma, ni wazi kuwa huduma tunayotoa wapo wenzetu wanatambua na kuthamini tunachokifanya na ndiyo maana wameamua kuja kujifunza na kupata uzoefu,” amesema Mhe. Kikwete

Amesema anaamini uzoefu ambao Somalia itaupata kupitia ziara hiyo utasaidia kuboresha zaidi masuala ya utumishi wa umma nchini humo.

Mhe. Kikwete amesema ujumbe huo unapata fursa ya kujifunza maeneo mbalimbali, ikiwemo namna Serikali inavyohusiana na wananchi, uratibu wa masuala ya kazi na ajira, usalama wa wafanyakazi mahali pa kazi pamoja na mifumo ya pensheni kwa watumishi wanaostaafu katika taasisi za Serikali na sekta binafsi.

“Hii ziara ni kielelezo tosha kuwa Somalia imedhamiria, ndiyo maana haijaweza kutuma maafisa pekee, lakini Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma ameamua kuja mwenyewe na timu yake kwa lengo la kujifunza na kuja kuona kwa macho yake kazi kubwa iliyofanyika Tanzania,” amesisitiza Mhe. Kikwete

Kwa upande wake, Mhe. Ganni amesema ujumbe wake umefika Tanzania kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika masuala ya utumishi wa umma, hususan matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuboresha utoaji wa huduma.

Amesema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika utoaji wa huduma kwa wananchi, huku watumishi wa umma wakitumia mifumo ya kidijitali kuwahudumia wananchi na kuhakikisha wanapata haki zao.

Mhe. Ganni amesema ujio wao ni muhimu kutokana na hatua ambazo Tanzania imepiga katika kuboresha utendaji wa Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema wamevutiwa pia na namna mifumo ya Serikali inavyowawezesha watumishi kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Akizungumzia mfumo wa e-Mrejesho, Mhe.Ganni amesema ni miongoni mwa mifumo waliyoona ina umuhimu katika kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, hivyo wanatarajia kujifunza namna unavyofanya kazi na uwezekano wa kutumia uzoefu huo katika kuboresha huduma nchini Somalia.

Ziara hiyo ya ujumbe wa Somalia inalenga pia kujifunza kuhusu mifumo ya Baraza la Mawaziri, usimamizi wa rasilimali watu, uajiri kwa kuzingatia sifa, Serikali mtandao, usimamizi wa ajira na mifumo ya taarifa za soko la ajira.

Ujumbe huo pia unatarajiwa kutembelea Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kwa ajili ya kujionea namna shughuli za Serikali zinavyoratibiwa na kutekelezwa.








Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »