WASIRA ATAKA WANA CCM WAKUTANE, WASIINGIE MKENGE KWA MANENO YA MITANDAONI.

August 19, 2026

Mwenyekiti wa Chama cha CCM Bara Ndugu Stephen Wasira, Akizungumza na wanachama wa CCM Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakati wa kuanza ziara rasmi ya kikazi ya kukagua uhai wa chama Mkoani humo

_Na Mwandishi Wetu - Singida_

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndugu Stephen Wasira, amewataka wanachama wa CCM kukutana mara kwa mara katika vikao rasmi vya chama ili kujadili masuala muhimu na kuepuka kupotoswa na taarifa zisizo na ukweli zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza leo tarehe 19 Agosti, 2026 Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakati wa kuanza ziara rasmi ya kikazi ya kukagua uhai wa chama, Wasira amesema vikao hivyo vinawapa wanachama fursa ya kupata taarifa sahihi na kuambizana ukweli.

"Wanachama wetu nchi nzima, kwa mujibu wa Katiba mna vikao vya wanachama. Mkutane muambizane. Siku hizi kwenye mitandao kuna uongo mwingi sana. Usipoangalia unaweza hata wewe kushirikishwa kusema uongo," amesema.

Amesisitiza kuwa ni muhimu wanachama kukutana na kujadili madai yanayosambaa, kisha kumtafuta mtu mwenye ujuzi awasaidie kuyafafanua.

"Kwa hiyo ni vizuri kukutana mkasema hili jambo limesemwa sana, maana yake ni nini? Mkamwita mtu anayejua akawasaidia kufafanua," ameeleza.

Makamu Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa mikutano ya wanachama ni fursa muhimu ya kujadili masuala yanayoendelea nchini ili waweze kukitetea chama ipasavyo.

Kuhusu uhuru na umoja wa nchi, Wasira amesema CCM itaendelea kulinda urithi huo uliopatikana kwa kazi kubwa.

"Hii ndiyo CCM. Kazi ya kwanza tulipewa ni uhuru na tunalinda. Ya pili ni umoja na tunahakikisha unabaki. Yeyote anayetaka kuubomoa anabomoa msingi ambao hawezi. Anaweza kutikisa matawi lakini mizizi itabaki chini," amesema.


Ameongeza kuwa wapo wanaodai CCM haijatekeleza chochote tangu uhuru, jambo ambalo amelisema ni kinyume na ukweli.

"Wanasema hatujafanya chochote tangu uhuru. Lakini uhuru wa kusema ndio huo walionao. Mdomo una kazi mbili: kusema na kula. Mtu akisema hakuna chochote tangu uhuru, muache tu. Huyo ana matatizo anahitaji msaada," amehitimisha.

---




Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »