UNESCO: VIJANA TUMIENI UBUNIFU KUIJENGA TANZANIA YA 2050

August 17, 2026

 




Na Oscar Assenga, Tanga


TUME ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza umuhimu wa vijana kutumia elimu, sayansi na ubunifu katika kutengeneza suluhisho za changamoto mbalimbali za jamii, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa Tume hiyo, Julitha Mlay katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara Jijini Tanga kunakofanyika maonesho ya wiki ya Kitaifa ya Elimu,Ubunifu na Ujuzi, ambapo amesema tume hiyo imeamua kushiriki maonesho hayo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za wabunifu na kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli zake.

Mlay amesema ubunifu unapaswa kupewa kipaumbele katika ngazi zote, akieleza kuwa vijana wanapaswa kuhamasishwa kupenda masomo ya sayansi na kutumia vipaji na uwezo wao kutengeneza vitu vinavyoweza kusaidia jamii.

“Tumekuja kushiriki maonesho haya kwa sababu tunatambua umuhimu wa ubunifu na tunataka kuwasapoti wabunifu, hasa vijana, kwa sababu ubunifu unahitajika katika ngazi zote za maendeleo,” amesema Mlay.

Amesema moja ya majukumu ya tume hiyo ni kutoa elimu kwa umma ili wananchi waweze kutofautisha kati ya Tume ya Taifa ya UNESCO na UNESCO ya Umoja wa Mataifa, ambazo mara nyingi huchanganywa.

Kwa mujibu wa Mlay, Tume ya Taifa ya UNESCO inatekeleza majukumu yake katika maeneo makuu matano ambayo ni elimu, sayansi za asili, sayansi za jamii, utamaduni na urithi wa dunia, pamoja na mawasiliano na habari.

Amesema ushiriki wao katika maonesho hayo pia unalenga kuwafikia wananchi na kuwaeleza nafasi ya UNESCO katika kuchochea maendeleo kupitia elimu, sayansi, utamaduni, mawasiliano na ubunifu.

Mlay amewataka vijana kuachana na mtazamo wa kutegemea mbinu za zamani pekee na badala yake kuendelea kubuni njia mpya zitakazowezesha taifa kuongeza kasi ya maendeleo.

Amesema vijana wanapaswa kutambua vitu wanavyovipenda na kuvifanyia kazi kwa bidii, huku wakitumia elimu ya sayansi na teknolojia kuboresha mawazo yao na kuyageuza kuwa bidhaa au suluhisho zenye manufaa kwa jamii.

“Vijana wapende masomo ya sayansi na waangalie kile kitu wanachokipenda, kisha waongeze bidii zaidi. Hapo ndipo wanapoweza kujijenga na kuchangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambao utekelezaji wake umeanza sasa,” amesema.

Amesema Tanzania inahitaji kizazi chenye uwezo wa kufikiri kwa ubunifu, kutumia maarifa na teknolojia katika kutatua changamoto na kujenga fursa mpya za kiuchumi na kijamii.

Kwa msingi huo, amesema taasisi mbalimbali zinapaswa kuendelea kutoa mazingira rafiki kwa vijana na wabunifu ili mawazo yao yaweze kukua na kutumika katika kuleta maendeleo ya taifa.

Tume ya Taifa ya Unesco ina jukumu la kuratibu shughuli zote za Unesco hapa nchini na imekuwa kiungo na daraja rasmi la kisheria la mawasiliano na kiutendaji linalounganisha serikali ya Tanzania na UNESCO.

Pia Tume hiyo inahamasisha ushiriki wa serikali na zisizo za serikali na wadau mbalimbali katika kuandaa na kutekeleza program za unesco hapa nchini ikiwemo kutoa ushauri wa kitaalamu kwa serikali kuhusu maswala yaliyondani ya unesco ikiwemo elimu sayansi utamaduni mawasiliano na habari ikiwa ni pamoja na kuratibu ushiriki wa Tanzania katika mikutano na shughuli za Unesco na kushirikianana ujumbe wa Tanzania katika mikutano ya UNESCO

mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »