TPDC YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA PUMP STATION NAMBA 3-MRADI WA EACOP

August 07, 2026
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema linaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Pump Station Namba 3 (PS3) wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unaotekelezwa katika Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.

Mkurugenzi wa Uwekezaji na Mipango wa TPDC, Bw. Derick Moshi, amesema ujenzi wa kituo hicho umefikia zaidi ya asilimia 88 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Agosti au mwanzoni mwa Septemba 2026.

“Tunawashukuru wakandarasi kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwa sasa ujenzi wa kituo hiki umefikia zaidi ya asilimia 88 na tunatarajia kitakamilika mwezi Septemba 2026,” amesema Bw. Moshi.

Ameeleza kuwa Pump Station Namba 3 ni moja ya miundombinu muhimu katika utekelezaji wa Mradi wa EACOP, kwani ndicho kituo cha kwanza upande wa Tanzania kitakachopokea mafuta ghafi kutoka Uganda na kuanza kuyasukuma kupitia bomba kuelekea Bandari ya Tanga kwa ajili ya usafirishaji.

Kwa mujibu wa Bw. Moshi, utekelezaji wa mradi huo umeendelea kuwa mfano bora wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kufanikisha miradi mikubwa ya kimkakati.

“Mradi huu umekuwa shamba darasa na kielelezo katika utekelezaji wa miradi mikubwa, hususan katika ushirikishwaji baina ya Serikali, sekta binafsi na wananchi. Tunategemea kutumia uzoefu huu katika miradi mingine ijayo,” amesema.

Amesema maendeleo yaliyofikiwa yanaonyesha dhamira ya Serikali na wadau wa mradi kuhakikisha miundombinu yote muhimu inakamilika kwa wakati ili kuanza shughuli za usafirishaji wa mafuta kama ilivyopangwa.

Kwa mujibu wa TPDC, ujenzi wa vituo vyote vya kusukuma mafuta vya Mradi wa EACOP unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026, huku usafirishaji wa mafuta ghafi kupitia bomba hilo ukitarajiwa kuanza Februari 2027.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »