TOL GASES YAWEKA WAZI UWEZO WA TANZANIA KUZALISHA OKSIJENI YA TIBA

August 17, 2026
Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeombwa kuzipa kipaumbele kampuni binafsi zenye uwezo wa kuzalisha oksijeni ya tiba kwa ajili ya matumizi hospitalini, badala ya kuwekeza zaidi katika uzalishaji wake, ili kutumia kikamilifu uwezo uliopo nchini.

Ombi hilo limetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TOL Gases PLC, Daniel Warungu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa 31 wa Mwaka wa Wanahisa wa kampuni hiyo.

Warungu amesema TOL Gases ina uwezo mkubwa na imebobea katika uzalishaji wa oksijeni ya tiba, hivyo Serikali inaweza kununua gesi hiyo kutoka kwa wazalishaji binafsi na kuelekeza rasilimali katika maeneo mengine muhimu ya sekta ya afya.

“Tunafanya uwekezaji mkubwa unaowezesha kuzalisha gesi ya oksijeni kwa ajili ya kuhakikisha kunakuwa na hewa tiba kwa ajili ya hospitalini. Ombi letu Serikali badala ya nayo kuwa inazalisha, iweke utaratibu wa kuwa inanunua kutoka sekta binafsi,” amesema.

Amesema hatua hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotambua umuhimu wa sekta binafsi kuwa mshirika muhimu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wa utendaji wa kampuni, Warungu amesema mapato ya TOL Gases yaliongezeka kutoka Sh bilioni 30.2 mwaka 2024 hadi Sh bilioni 31.15 mwaka 2025.

Amesema EBITDA iliongezeka kutoka Sh bilioni 10.5 hadi Sh bilioni 13.4, huku faida kabla ya kodi ikipanda kutoka Sh bilioni 3.98 hadi Sh bilioni 6.78.

Ameongeza kuwa TOL Gases inaendelea kuongeza uwezo wa uzalishaji kupitia miradi mikubwa miwili, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha Ikama III cha kuzalisha hewa ya ukaa (Carbon Dioxide), kinachotarajiwa kuanza uzalishaji Septemba 2027.

Aidha, kampuni inajenga kituo kipya cha kutenganisha hewa (ASU) kwa msaada wa Clinton Health Access Initiative (CHAI), kinachotarajiwa kuanza kufanya kazi Oktoba 2026 na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa oksijeni hadi takribani tani 20 kwa siku.

Warungu amesema uwekezaji huo utaongeza ufanisi wa uzalishaji, kurahisisha matengenezo ya mitambo na kuongeza uwezo wa kukidhi mahitaji ya gesi katika sekta ya afya na viwanda.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TOL Gases, Leonard Kitoka, amesema Tanzania kwa sasa ina uwezo wa kutosha kutoka kwa wazalishaji binafsi kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo ya oksijeni ya tiba kutokana na uwekezaji uliofanyika katika mitambo ya uzalishaji.

Kuhusu Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Kitoka amesema thamani ya hisa za TOL Gases imeongezeka kutoka Sh 795 wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka uliopita hadi kufikia Sh 1,490, sawa na ongezeko la takribani asilimia 74. Kwa sasa, hisa hizo zinauzwa kati ya Sh 1,320 na Sh 1,490.

Amesema kampuni inapendekeza hospitali na vituo vya afya kuwezeshwa kununua oksijeni yenye ubora unaohakikishwa kutoka kwa wazalishaji binafsi waliopo nchini.

Kwa mujibu wa Kitoka, hatua hiyo itasaidia kutumia kikamilifu uwezo wa uzalishaji uliopo, kuepusha uwekezaji unaojirudia na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa oksijeni ya tiba kwa gharama nafuu.

Amesema TOL Gases itaendelea kushirikiana na Serikali, taasisi za afya na wadau wa maendeleo kuhakikisha upatikanaji wa oksijeni salama na yenye ubora nchini, sambamba na kuendelea kuwekeza katika uzalishaji, usambazaji na utaalamu wa kiufundi.

Katika hatua nyingine, amesema wanahisa wamekubaliana kwa kauli moja kutogawana gawio la faida kwa sasa, badala yake fedha hizo kuelekezwa katika ujenzi wa miundombinu na uwekezaji wa kampuni kwa lengo la kuongeza uwezo wa uzalishaji na mapato.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »