SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA WAZEE: WAZIRI SANGU

August 06, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, akizungumza na Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Lindi tarehe 5 Agosti, 2026. Waziri Sangu aliwahakikishia wazee hao kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inathamini na kujali maslahi yao.

*************

Na: OWM (KAM), Lindi

Serikali imesema itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa wazee katika kujenga jamii yenye amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Amesema hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) Mhe. Deus Sangu Agosti 5, 2026 alipokutana na wajumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Lindi katika kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Aidha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwamo wazee, ili kuhakikisha sauti zao zinasikika na changamoto zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi.

Vile vile, Waziri Sangu alieleza kuwa kuanzishwa kwa jukumu la Mahusiano ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni sehemu ya juhudi za Serikali za kujenga mawasiliano ya karibu na wananchi pamoja na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Kadhalika aliwataka wazee waendelee kutumia busara, hekima na uzoefu wao kuwaongoza vijana katika kuzingatia maadili mema, uzalendo na kuhifadhi historia ya taifa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

“Ninyi mmeiona Tanzania katika awamu mbalimbali za uongozi. Tunaomba muendelee kuwafundisha vijana historia ya nchi yetu na kuwajengea uzalendo ili amani na mshikamano viendelee kudumu,” alisema Sangu.

Kwa upande mwengine, Waziri Sangu amewaahidi kuyafikisha serikalini maoni yao kuhusu masuala ya pensheni, bima ya afya na ushiriki katika vyombo vya maamuzi ili yafanyiwe kazi.

Katika kikao hicho, wajumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee waliwasilisha hoja nane wakitaka Serikali kuboresha ustawi wao, ikiwamo kuanzisha pensheni kwa wazee wasiokuwa watumishi wa umma, kuimarisha huduma za bima ya afya, utoaji wa vitambulisho na kuongeza ushiriki wao katika mabaraza ya maamuzi ya wilaya na mkoa.

Katibu Msaidizi wa Baraza hilo, Salum Mchola alisema wazee wengi wanaishi katika mazingira magumu baada ya kumaliza nguvu za kufanya kazi, hivyo wanaamini mfumo wa pensheni kwa wazee wote unaweza kusaidia kuboresha maisha yao kama ilivyo Zanzibar.

“Tunaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuanzisha pensheni kwa wazee wote, hususan wale ambao hawakuwahi kuajiriwa serikalini. Huu ni mfumo unaoweza kuigwa kutoka Zanzibar,” alisema Mchola.

Akijibu hoja hizo, Waziri Sangu alisema maoni yote yaliyowasilishwa yatafikishwa kwa wizara husika, ikiwamo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, ili yajadiliwe na kupatiwa mwelekeo wa kisera.

Alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kutafuta njia za kuboresha ustawi wa wazee na kwamba ushauri wao ni muhimu katika kujenga mahusiano bora kati ya Serikali na wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, alisema mkoa huo una takribani wazee 120,000 wenye umri wa miaka 60 na kuendelea sawa na asilimia nane ya wakazi wote wa mkoa huo.

Mwanziva alisema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha maisha ya wazee, huku akiwataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi za kuimarisha maendeleo na mshikamano wa taifa.

Aliongeza kuwa wazee bado ni hazina ya maarifa na uzoefu unaohitajika katika jamii, akisema ushauri wao una mchango mkubwa katika malezi ya vijana, utatuzi wa migogoro na kuendeleza maadili ya Kitanzania.

Waziri Sangu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Lindi ambapo leo anatarajiwa kutembelea kituo cha kulelea wazee wenye uhitaji, kukagua miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Lindi na kutembelea mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »