PINDA APONGEZA TVLA KWA KUJENGA UWEZO WA NDANI WA KUZALISHA CHANJO ZA MIFUGO

August 06, 2026
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (wa pili kutoka kushoto), akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Japhet Nkangaga kuhusu huduma zinazotolewa na TVLA, wakati alipotembelea banda la TVLA lililopo kwenye banda jumuishi la Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Maonesho ya Kilimo ya NaneNane 2026 yanayoendelea kwenye Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Prof. Mohammed Ali Sheikh.

*****************

Na Daudi Nyingo – Dodoma

Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda ameipongeza Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa hatua ya kujenga uwezo wa ndani wa kuzalisha chanjo za mifugo, akisema hatua hiyo imeisaidia Tanzania kupunguza utegemezi wa chanjo kutoka nje ya nchi na kutumia wataalamu wake katika kulinda afya ya mifugo.

Mhe. Pinda ameyasema hayo leo Agosti 6, 2026 alipofanya ziara katika banda la TVLA lililopo kwenye banda jumuishi la Wizara Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakati wa Maonesho ya Kilimo ya NaneNane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.

Mara baada ya kupata maelezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na TVLA, Mhe. Pinda alisema hatua iliyofikiwa na TVLA inaonyesha uwezo mkubwa wa wataalamu wa ndani katika kuhakikisha sekta ya mifugo inaendelea kuimarika na kupunguza utegemezi wa huduma muhimu kutoka nje ya nchi.

“Mimi nadhani kizuri hapa kwa Wizara ni kuwapongeza na kujipongeza tu. Maana mambo yale yote nimeyaona pale, zamani tulikuwa tunatoa chanjo za mifugo nje ya nchi. Kwa hiyo unajua oh sasa labda chanjo zenyewe hazipatikani au zimepungua. Lakini kumbe vitu hivi viko ndani ya uwezo. Wataalamu wetu tunao kabisa,” amesema Mhe. Pinda.

Ameongeza kuwa uwezo wa kuzalisha chanjo nchini ni hatua muhimu katika kulinda rasilimali za taifa kwa kuwa fedha ambazo zingetumika kuagiza huduma hizo kutoka nje zinaweza kuelekezwa kwenye maeneo mengine ya maendeleo.

“Kwa hili kwa kweli mnastahili pongezi kabisa maana mmenusuru vidola vyetu vya kimasikini hivi, vingeliendelea tu kwenda nje,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Prof. Mohammed Ali Sheikh amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika udhibiti wa magonjwa ya mifugo kwa kuhakikisha wanyama wanapata chanjo salama na zenye ubora.

Prof. Sheikh amesema katika kampeni ya kitaifa ya chanjo za mifugo, Serikali ilitoa zaidi ya Shilingi bilioni 260 kwa ajili ya kuhakikisha mifugo nchini inapata kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, huku TVLA ikiwa miongoni mwa taasisi muhimu zilizoshiriki katika utekelezaji wa mpango huo.

Amesema TVLA imeendelea kuisaidia Serikali kwa kuzalisha na kusambaza chanjo zinazokidhi mahitaji ya wafugaji na kuhakikisha chanjo zinazotolewa kwa mifugo zinakuwa salama na zenye ubora unaohitajika.

“Taasisi yetu ya ndani ya Serikali inayoaminika, TVLA, ilitoa chanjo ikiwa miongoni mwa kampuni ambazo ziliingia mikataba ya kusambaza chanjo hizi kwa ajili ya wanyama wetu. Kwa hiyo, wanafanya kazi kubwa na wanaisaidia sana Serikali na inatueka kuwa na uhakika kwamba chanjo zetu ni salama,” amesema Prof. Sheikh.

Akitoa maelezo kuhusu uwezo wa uzalishaji wa chanjo, Meneja wa TVLA Dodoma, Dkt. Japhet Nkangaga amesema Wakala imejipanga kuzalisha jumla ya dozi milioni 129.3 za chanjo za mifugo mbalimbali kwa mwaka huu kulingana na mahitaji ya taifa.

Amesema kati ya hizo, dozi milioni 120 zitatengwa kwa ajili ya chanjo ya kuku dhidi ya ugonjwa wa Mdondo, huku dozi nyingine zikihusisha chanjo mbalimbali kwa wanyama wengine.

“Katika chanjo zetu mwaka huu tunampango wa kutengeneza dozi milioni 129 na laki tatu (129,300,000) ambazo ni za wanyama mbalimbali. Lakini ikiwepo kuku ni dozi milioni 120 kwa sababu Tanzania nzima, chanjo ya kuku kwa maana ya kukinga dhidi ya Mdondo, inahitajika zaidi,” amesema Dkt. Nkangaga.

Ameeleza kuwa uzalishaji wa chanjo hufanyika kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wafugaji kutokana na ukweli kwamba chanjo zina muda maalumu wa matumizi.

“Tunafanya hivyo kwa sababu hizi chanjo zetu zinakuwa na muda wa kuharibika. Sasa tukitengeneza nyingi zinaweza kuharibika pale muda ukifika kama hazijatumika. Kwa hiyo mahitaji yetu yanasaidia kutengeneza kitu ambacho tunahitaji,” amesema.

Dkt. Nkangaga amesema mbali na uzalishaji wa chanjo, TVLA pia inajihusisha na uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama, utafiti wa magonjwa na wadudu wanaoeneza magonjwa hayo, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, usajili na udhibiti wa ubora wa viuatilifu vya mifugo pamoja na kutoa huduma za ushauri na mafunzo kwa wadau wa sekta ya mifugo.

Katika ziara hiyo, Dkt. Nkangaga alimweleza Mhe. Pinda umuhimu wa uchunguzi wa magonjwa ya mifugo kwa kuonyesha baadhi ya sampuli za kondoo waliopata tatizo la kutupa mimba kutokana na ugonjwa unaoweza kuzuilika kwa njia ya chanjo.

Amesema matukio hayo yanaonesha umuhimu wa wafugaji kutumia huduma za uchunguzi na chanjo kwa wakati ili kuepuka hasara zinazotokana na magonjwa ya mifugo.

Maonesho ya NaneNane 2026 yanaendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, huku TVLA ikiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake.
Matukio mbalimbali  wadau wa sekta ya mifugo wakitembelea banda la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), lililopo kwenye banda jumuishi la Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakipata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na TVLA ikiwemo uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo, uzalishaji na usambazaji wa chanjo, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo pamoja na huduma nyingine za maabara, wakati wa Maonesho ya Kilimo ya NaneNane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Japhet Nkangaga kuhusu uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo pamoja na huduma nyingine za maabara zinazotolewa na TVLA, wakati alipotembelea banda la TVLA kwenye Maonesho ya Kilimo ya NaneNane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Japhet Nkangaga kuhusu uwezo wa Wakala hiyo katika kuzalisha chanjo za mifugo, ambapo mwaka huu TVLA imejipanga kuzalisha jumla ya dozi milioni 129.3 za chanjo mbalimbali kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya taifa, wakati wa ziara yake katika banda la TVLA kwenye Maonesho ya Kilimo ya NaneNane 2026 yanayoendelea jijini Dodoma.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »