Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mfumo wa Supervisory Control and Data Acquisition (SCADA) yameimarisha udhibiti wa upotevu wa mafuta wakati wa shughuli za ushushaji kutoka melini kwenda kwenye maghala ya kuhifadhia.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mhandisi wa PBPA, Bi. Elvira Muganga, alisema mfumo huo unaiwezesha Serikali kufuatilia kwa wakati halisi kiwango cha mafuta kinachopokelewa nchini.
Alisema SCADA hukusanya taarifa kutoka kwenye mita za Serikali zilizowekwa katika maeneo ya kupokelea mafuta na kuziwezesha kulinganishwa na taarifa za mita zilizopo kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta.
“Ulinganishaji huu unasaidia kubaini tofauti zinazoweza kujitokeza wakati wa ushushaji na kuhakikisha kiasi cha mafuta kilichopokelewa kinarekodiwa kwa usahihi,” alisema Bi. Muganga.
Alieleza kuwa kabla ya matumizi ya teknolojia hiyo, ufuatiliaji wa shughuli za ushushaji wa mafuta ulikuwa unategemea zaidi taarifa zilizokusanywa kwa njia zisizo za moja kwa moja. Mfumo wa SCADA sasa umeongeza uwezo wa Serikali kupata taarifa sahihi kwa wakati na kusimamia operesheni hizo kwa karibu.
Kwa mujibu wa Muganga, udhibiti huo umeongeza uwazi na usalama katika mapokezi ya mafuta pamoja na kuimarisha usahihi wa taarifa zinazotumika katika ukokotoaji wa mapato ya Serikali.
Aidha, alisema matumizi ya mfumo huo yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotumia teknolojia ya kidijitali kusimamia mapokezi ya bidhaa za mafuta na kudhibiti upotevu unaoweza kutokea wakati wa ushushaji.
Muganga alisema PBPA inatumia Maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utendaji wa mfumo huo na mchango wake katika kuhakikisha mafuta yanayoingia nchini yanasimamiwa kwa uwazi na ufanisi.
Aliwahimiza wananchi na wadau wa sekta ya nishati kutembelea banda la PBPA ili kufahamu zaidi kuhusu mfumo wa SCADA, Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja na majukumu mengine ya Wakala.

EmoticonEmoticon