MFUMO WA M+2 WAIMARISHA UHAKIKA WA MAFUTA NCHINI

August 06, 2026

DODOMA

Mfumo wa kuagiza mafuta kwa ajili ya matumizi ya miezi miwili inayofuata umeiwezesha Tanzania kuendelea kuwa na bidhaa za mafuta za kutosha, licha ya vita na changamoto nyingine zinazoathiri soko la dunia.

Hayo yameelezwa na Mhandisi Rehema Mahundi katika siku ya sita ya Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

Mhandisi Mahundi alisema moja ya maswali yanayoulizwa zaidi na wananchi ni namna Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja unavyoiwezesha nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta, hasa wakati wa migogoro na vita katika maeneo mbalimbali duniani.

Akijibu swali hilo, alieleza kuwa PBPA hutangaza zabuni kila mwezi kwa ajili ya kuagiza mafuta yatakayotumika nchini katika miezi miwili inayofuata. Utaratibu huo unajulikana kama M+2.

“PBPA huingia mikataba na wazabuni walioshinda zabuni hizo ili kuhakikisha bidhaa za mafuta zinafika nchini kwa wakati, hata changamoto zinapojitokeza katika soko la dunia,” alisema Mhandisi Mahundi.

Alisema kupitia mfumo huo, Tanzania imeendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta wakati wote na kwa gharama zinazoakisi hali halisi ya soko la dunia.

Katika Maonesho ya Nanenane, PBPA imeendelea kutoa elimu kuhusu Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja kwa watu kutoka makundi mbalimbali, wakiwamo wanafunzi, wakulima, wajasiriamali, wafanyabiashara pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za elimu na sekta binafsi.

Mhandisi Mahundi amewakaribisha wananchi kutembelea Banda la PBPA katika Viwanja vya Nanenane jijini Dodoma ili kupata elimu zaidi kuhusu namna mfumo huo unavyosimamia mnyororo wa uagizaji, usimamizi na upokeaji wa bidhaa za mafuta nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »