MTAKUWWA YAZINDUA KAMPENI Ya 'AMSHA ARI' MIRONGO KUHAMASISHA KUPINGA UKATILII KWA WANAWAKE NA WATOTO

June 27, 2026

 




Mwanza. Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wanawake na Watoto Mkoa wa Mwanza (MTAKUWWA) imezindua kampeni ya Amsha Ari katika Kata ya Mirongo, ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kushiriki katika malezi bora ya watoto, kuzuia mmomonyoko wa maadili na kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Uzinduzi wa kampeni hiyo uliwashirikisha waendesha bodaboda wa Kata ya Mirongo, ambao walieleza utayari wao wa kushiriki kikamilifu katika kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuhamasisha ulinzi wa makundi hayo.

Aidha, waendesha bodaboda hao waliitaka jamii kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini na kuwahimiza vijana kuepuka kutumika katika vitendo vya uchochezi vinavyoweza kuhatarisha usalama wa wananchi na mali zao.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti Mwenza wa MTAKUWWA Mkoa wa Mwanza, Yassin Ally, aliwataka waendesha bodaboda kuwa mstari wa mbele katika kufichua vitendo vya ukatili, kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari zake na kushiriki kulinda maadili ya jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa MTAKUWWA Mkoa wa Mwanza, akiwemo Twaha Bakari, ambaye ni kiongozi wa dini, na Fatuma Mpinga, Mkaguzi wa Polisi wa Kata ya Mirongo, walisisitiza umuhimu wa kampeni hiyo kwa kuhimiza jamii kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto, kulinda maadili na kuendeleza amani ya nchi.




Share this

Related Posts

Previous
Next Post »