WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan itaendelea kulinda ajira zilizopo na kuzalisha ajira mpya kupitia sekta ya viwanda na biashara kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Kapinga amesema hayo Mei 8, 2026 jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Kiwanda cha Nguo cha Tooku Garments kilichopo Ubungo External, akieleza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kujiridhisha na utendaji wa viwanda nchini pamoja na kupanua wigo wa biashara na uwekezaji.
Amesema kiwanda hicho kimeajiri takribani vijana 7,000, ambapo asilimia 75 ya wafanyakazi ni wanawake huku asilimia 60 wakiwa vijana wenye umri chini ya miaka 30, hatua aliyosema inaonesha mchango mkubwa wa viwanda katika kupunguza tatizo la ajira nchini.
Aidha, Waziri Kapinga amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda ikiwemo miundombinu na huduma muhimu, ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tooku Garments, Borja Trenor Casanova amesema kiwanda hicho ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mpango wa African Growth and Opportunity Act (AGOA) nchini, huku kikiwa miongoni mwa wasafirishaji wakubwa wa mavazi kwenda Marekani.
Amesema kwa sasa wanaendelea kushinikiza kuongezwa kwa muda wa AGOA kwa miaka 10 hadi 20 zaidi ili kuchochea uwekezaji na kukuza ajira nchini, akibainisha kuwa iwapo mpango huo utafanikiwa, kampuni hiyo inalenga kuongeza idadi ya wafanyakazi hadi kufikia 30,000.
EmoticonEmoticon