STARTUPS ZAASWA KUONGEZA UBORA WA BIDHAA ILI KUCHOCHEA UCHUMI WA TAIFA

May 06, 2026
Dar es Salaam, Mei 5, 2026

Kampuni changa (startups) nchini waaswa kuongeza juhudi katika kukuza ubunifu na kuugeuza kuwa bidhaa ama huduma zenye ushindani, hatua iliyotajwa kuwa mhimili muhimu wa kukuza uchumi wa taifa na kuimarisha ajira kwa vijana.

Wito huo umetolewa wakati wa uzinduzi wa iMbeju - UDSM Startups Challenge, uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hafla hiyo imewakutanisha wabunifu, wawekezaji, taasisi za kifedha pamoja na wadau wa maendeleo, wakijadili namna bora ya kuendeleza mawazo ya kibunifu hadi kufikia hatua ya ubiasharishaji

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika ubunifu na ujuzi kwa vijana, akieleza kuwa hatua hiyo ni nyenzo madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya ajira nchini.

“Ubunifu ni injini ya uchumi wa kisasa. Tunapowawezesha vijana wetu kuwa wabunifu, tunajenga taifa linalojitegemea kiuchumi na lenye ushindani kimataifa,” alisema Prof. Mkenda.

Aliongeza kuwa Vyuo Vikuu vina wajibu wa kuwa vitovu vya ubunifu kwa kufanya tafiti zenye tija ili kuweza kupata bunifu zinazoweza kuzalisha ajira na kuchochea maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, aliwahimiza wabunifu kutumia kikamilifu fursa za kifedha zinazotolewa kupitia ushirikiano kati ya COSTECH na CRDB Bank, hususan mfuko wa Samia Commercialization Fund .

“Ninyi watafiti na wabunifu, hizi ni fedha zenu. Hata kama unahitaji mtaji mkubwa, kuna mikopo yenye masharti nafuu itakayowezesha kukuza biashara zenu,” alisema Dkt. Nungu.

Alisisitiza kuwa changamoto ya mtaji isiwe kikwazo, bali iwe motisha ya wabunifu kujitokeza na kuwasilisha miradi yao kwa ajili ya ufadhili, ili mawazo yao yaweze kufikia hatua ya uzalishaji na kuingia sokoni.

Imbeju - UDSM Startups Challange hiyo imehusisha wabunifu mbalimbali waliowasilisha (showcase) bidhaa na huduma bunifu mbele ya wadau wa maendeleo, wawekezaji na taasisi za kifedha. Hatua hiyo inatarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji na kukuza kampuni changa, huku ikiimarisha nafasi ya ubunifu kama kichocheo cha maendeleo ya uchumi nchini.

Kwa ujumla, iMbeju – UDSM Startups Challenge imeonesha wazi kuwa ubunifu unaendelea kuwa nguzo muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda na maarifa.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »