USHINDANI WA HAKI WAFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI TANZANIA

May 14, 2026
SERIKALI imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kupitia kuimarisha sera za ushindani wa haki zinazosaidia biashara kushindana kwa uwazi, kuongeza ubunifu na kuwalinda walaji.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi, wakati akifungua Mkutano wa Sheria za Ushindani na Wawekezaji Tanzania ulioandaliwa kujadili nafasi ya ushindani wa haki katika kukuza uwekezaji na uchumi wa taifa.

Amesema Tanzania inaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa uchumi sambamba na kuongezeka kwa viwanda pamoja na ushiriki katika masoko ya kikanda na kimataifa, hali inayohitaji kuwepo kwa mifumo imara ya ushindani wa haki ili kuhakikisha maendeleo hayo yanaleta manufaa kwa wananchi wote.

Aidha amesema sera za ushindani zimekuwa sehemu muhimu ya mageuzi ya uchumi kwa kuwa zinasaidia biashara kushindana kwa haki, kulinda maslahi ya walaji na kuhamasisha ubunifu katika sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma.

“Tanzania inaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa uchumi huku viwanda vikikua na ushirikiano katika masoko ya kikanda na kimataifa ukiendelea kuongezeka. Hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha ukuaji huo unaenda sambamba na uwajibikaji na biashara za haki,” amesema.

Ameongeza kuwa sera imara za ushindani zinachangia kujenga imani kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa kuhakikisha masoko yanafanya kazi kwa uwazi, usawa na kuzingatia sheria zilizowekwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani wa Haki (FCC), Dkt. Aggrey Mlimuka, amesema ushindani wa haki na uwekezaji vina uhusiano mkubwa kwani wawekezaji huhitaji mazingira yenye uwazi na usawa ili kuweza kufanya biashara kwa uhakika.

“Ni vigumu kuvutia uwekezaji kama hakuna ushindani wa haki. Wawekezaji wanahitaji kuwa na uhakika kuwa wanafanya kazi katika mazingira ya soko yenye haki,” amesema.

Dkt. Mlimuka amesema mkutano huo umefungua jukwaa muhimu la kujadili namna sheria za ushindani zinavyoweza kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi Khadija Ngasongwa, amesema sheria za ushindani zina mchango mkubwa katika kuhakikisha biashara zinafanya kazi katika mazingira ya haki huku zikitoa nafasi kwa walaji kupata bidhaa na huduma bora.

Amesema sheria hizo zinaelekeza namna biashara zinavyoingia sokoni, zinavyopanga bei, kutangaza bidhaa na kushindana, hivyo kuwa sehemu muhimu ya kujenga uchumi wenye ushindani na uwazi.

Ngasongwa amesisitiza kuwa utekelezaji wa sheria za ushindani haupaswi kutafsiriwa kama kikwazo kwa biashara, bali ni msingi wa kujenga imani kwa wawekezaji na kuhakikisha ukuaji endelevu wa uchumi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »