SERIKALI YATOA BILIONI 48.8 BIMA YA AFYA KWA WOTE

May 11, 2026




Na Mwandishi Wetu , Dodoma


Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kaya zisizo na uwezo kwa kutoa Shilingi bilioni 48.8 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wa makundi maalum kupata huduma za afya kwa uhakika. Kupitia utekelezaji huo, jumla ya kaya 172,297 tayari zimefikiwa na kuingizwa kwenye mpango huo, huku wanufaika 463,228 wakianza kupata huduma mbalimbali za matibabu katika vituo vilivyosajiliwa nchini.

Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya Fungu 52 kwa mwaka 2026/27 Waziri wa Afya Mhe. Omary Mchengerwa amesema kuwa, utekelezaji huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kujali hali yake ya kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya safari ya kuelekea huduma jumuishi za afya kwa wananchi wote.

Katika kuimarisha sekta ya afya sambamba na utekelezaji wa mpango huo, mabaraza na bodi za kitaaluma yameendelea kusimamia ubora wa huduma kwa kusajili wataalam wa afya 14,310, hatua inayoongeza nguvu kazi muhimu kwa utoaji wa huduma nchini.

Amesema kuwa kuhusu upatikanaji wa huduma za matibabu, jumla ya maduka ya dawa 330 yamesajiliwa pamoja na watarajali 3,004, huku vituo vya kutolea huduma za afya 3,643 vikisajiliwa ili kuongeza upatikanaji wa huduma karibu na wananchi.

Katika kuhakikisha taaluma na maadili yanaendelea kuzingatiwa hususan wakati huu wa kuhudumia wananchi wengi zaidi kupitia mfumo wa Bima ya Afya, vituo binafsi vya afya 654 vimekaguliwa ili kuhakikisha vinakidhi viwango na kutoa huduma salama kwa wananchi.

Mafanikio hayo yanaakisi hatua kubwa ya Serikali katika kujenga mfumo imara wa afya unaojali usawa, ubora na upatikanaji wa huduma kwa wote, huku Bima ya Afya kwa Wote ikiendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »