SERIKALI KUIMARISHA NISHATI YA UMEME WILAYANI KONDOA

May 16, 2026




Katika jitihada za kuendeleza ustawi wa wananchi na kuchochea uchumi wa maeneo ya vijijni na vitongojini, Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme wilayani Kondoa kupitia mpango wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote vya wilaya hiyo.


 Mpaka sasa vitongoji 113 vina umeme huku kukiwa na mradi unaoendelea wa kupeleka umeme katika vitongoji 60.


Hayo yameelezwa leo Mei 16, 2026 na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba wilayani Kondoa, Dodoma.

Mhe. Salome ameeleza kwamba katika mradi wa umeme unaotekelezwa sasa wa kusambaza umeme katika vitongoji 60 zaidi ya shilingi billion 21 imetengwa kuhakikisha mradi huo unakamilika ambapo kukamilika kwake kutafanya  Kondoa kubakiwa na vitongoji 88 tu ambavyo havina umeme  vitakavyofikiwa na huduma hiyo ifikapo mwaka 2030.


Pia Mhe Salome ameeleza kwamba Serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni 752 kwa ajili ya  kuhakikisha wananchi ambao miradi ya umeme inapita karibu na nyumba zao  wanafikiwa na huduma ya umeme katika kaya zao.


Ameongeza kuwa katika Wilaya ya Kondoa,  Wizara ya Nishati ina mpango wa kubadilisha nguzo zote chakavu na kupeleka nguzo za zege ili kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa na nishati ya umeme ya uhakika ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi kama vile uendeshaji wa viwanda vidogo na shughuli za kijamii.

Vilevile amesema Serikali ina mpango mahsusi kujenga laini kubwa ya umeme ili kuimarisha na kutatua changamoto ya nguvu ya umeme (Low Voltage katika Jimbo la Kondoa).


Katika hatua nyingine, Mhe. Salome amewaasa wananchi kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia akieleza kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Wananchi Kondoa  kutunza misitu bado wanatakiwa kuilinda kwa kuachana na matumizi ya Kuni na mkaa na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kama vile gesi, umeme na mkaa mbadala 


“Niwahakikishie wanakondoa sasa hivi Serikali imeweka ruzuku katika mitungi ya gesi, hivyo niwaombee sana tuanze kutumia Nishati safi kwa ajili ya kulinda  afya, mazingira na kuokoa muda wa kukaa jikoni ili tuweze kujiendeleza kiuchumi lakini pia tutumie nishati nyingine kama mkaa mbadala usiotoa moshi ambapo utatumia mkaa kidogo kupika chakula kingi na katika hali iliyo bora zaidi." Amesisitiza  Mhe Salome.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »