NEMC, HALMASHAURI YA ILALA NA WADAU WA MAZINGIRA WASAFISHA FUKWE ZA DARAJA LA SALENDER

May 17, 2026
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ilala kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, JUZA, Care and Help, Chuo cha Maji, MUHAS pamoja na wadau mbalimbali wa mazingira wamefanya zoezi la usafi katika fukwe za Daraja la Salender zilizopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam. 

Zoezi hilo limehusisha ukusanyaji wa taka mbalimbali zilizokuwa zimetapakaa katika maeneo ya fukwe kwa lengo la kulinda mazingira na afya za wananchi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC), Bw. Elibariki Bajuta amesema ushirikiano kati ya taasisi na wananchi katika shughuli za usafi wa mazingira ni muhimu katika kuhakikisha maeneo ya pwani na vyanzo vya maji vinaendelea kuwa salama na endelevu.

“Uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu, hivyo tunapaswa kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira,” amesema Bajuta.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo amepongeza juhudi za NEMC na wadau walioshiriki katika zoezi hilo huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuacha tabia ya kutupa taka ovyo katika maeneo ya fukwe na mifereji ya maji.

“Tunapaswa kujenga utamaduni wa kutunza mazingira yetu kila siku ili kuyaacha salama kwa vizazi vijavyo,” amesema Mhe. Mpogolo.

Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira, uhifadhi wa maeneo ya pwani pamoja na kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaoweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu na viumbe hai wa baharini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »