Zoezi hilo la utiaji saini limefanywa na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Mhe. Dkt. Jimmy Gasore kwenye ukumbi wa mikutano wa Kigali Convention Center (KCC) unapofanyika Mkutano wa Pili wa Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA 2026) unaofanyika jijini Kigali, Rwanda.
Makubaliano hayo yanaangazia maeneo kadhaa ya ushirikiano ikiwemo kubadilishana umeme kati ya Tanzania na Rwanda ili kuimarisha usalama wa nishati, utekelezaji wa miradi ya pamoja ya miundombinu ya umeme, pamoja na kuendeleza biashara ya umeme baina ya nchi hizo mbili.
Aidha maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, usambazaji wa bidhaa za petroli, fursa zilizopo katika miradi ya LNG pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo akili bandia katika Sekta ya Nishati.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Fedha, Mhe Balozi Khamis Omar, Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Seif Pandu, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Felchesmi Mramba pamoja na wataalamu kutoka serikali zote mbili.






EmoticonEmoticon