Na OWM-SBUU -Morogoro
Serikali imezindua Kikosi Kazi cha Taifa cha Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji Taarifa (ME&R National Task Force) kwa lengo kuratibu utekelezaji wa Mwongozo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini katika kusimamia utendaji wa shughuli za Serikali.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 09 Aprili, 2026 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. James Kilabuko wakati akifungua Kikao Kazi Cha Kikosi Kazi cha Taifa cha Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji Taarifa (ME&R National Task Force) kilichofanyika mkoani Morogoro.
Dkt. Kilabuko amesema, Ufuatiliaji na Tathmini ni dhana muhimu ya usimamizi inayotumika kwa lengo la kuhakikisha uwajibikaji na uwazi katika utekelezaji wa afua za maendeleo.
“Kikosi Kazi hiki kitakuwa chombo cha kitaalamu cha kusaidia kuratibu utekelezaji wa Mwongozo Jumuishi wa U&Tc, kuoanisha mifumo ya kitaifa ya utendaji, kuimarisha ubora wa takwimu na taarifa za Serikali na kuandaa mapendekezo ya sera na maboresho ya kiutendaji” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Ameeleza kuwa, kikao kazi hicho ni fursa ya kipekee ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya namna bora ya kutekeleza majukumu ya Ufuatiliaji na Tathmini nchini.
“Matarajio yangu ni kwamba, baada ya kikao hiki tutaboresha uratibu na kuoanisha viwango vya kitaifa vya Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) katika Wizara, Idara na Wakala (MDAs), Sekretarieti za Mikoa (RSs) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) ni hatua muhimu katika kuhakikisha uwiano na ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo” amefafanua.
Vilevile, Dkt. Kilabuko amebainisha kuwa ipo haja ya kuoanisha viashiria vya taasisi na maeneo muhimu ya matokeo ya Kitaifa ili kuhakikisha kuwa juhudi za taasisi mbalimbali zinaendana na vipaumbele vya Taifa.
“ Katika hili, ni muhimu kuimarisha mwingiliano na utangamano wa Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi (PEPMIS), PIPMIS na Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo na Programu (NPMIS) ili kuwezesha mtiririko mzuri wa taarifa na matumizi ya data kwa ufanisi” ameeleza.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inataka kuona taarifa za U&T zikitumika kufanya maamuzi, miradi inakamilika kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha na maisha ya wananchi yanaboreshwa kutokana na kazi zinazotekelezwa.
“Haya yote yatawezekana ikiwa tutazingatia misingi ya Ufuatiliaji na Tathmini kama inavyoelekezwa katika Mwongozo Jumuishi. Tumieni muda huu vizuri kujadili masuala yatakayokuwa na maslahi mapana kwa nchi yetu na kuwa na Ufuatiliaji na Tathmini wenye tija” ameongeza Dkt. Kilabuko.
*MWISHO*










EmoticonEmoticon