DC MWANGA AZITAKA TAASISI ZOTE KUWEKA KIPAUMBELE KATIKA UPANDAJI MITI KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI

April 04, 2026


Wilaya ya Mwanga imeanza kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kufuatia wito wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Rukia Zuberi, aliyehimiza taasisi za serikali na sekta binafsi kupanda miti ya matunda na vivuli katika maeneo yao.


Wito huo umetolewa wakati wa zoezi la upandaji miti lililofanyika ofisini kwake, likiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Rukia Zuberi alisisitiza kuwa upandaji miti si tukio la muda mfupi, bali ni jukumu endelevu linalohitaji ushirikiano wa kila mwananchi na kila taasisi.



Alieleza kuwa miti ina mchango mkubwa katika kulinda mazingira, kuhifadhi udongo, na kupunguza athari za ukame pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa ndani ya wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.


Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya aliwahamasisha wananchi kutumia vizuri msimu wa mvua kwa kupanda miti na kuhakikisha wanaitunza hadi ikue. “Ni muhimu tuendelee kupanda miti na kuitunza kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema, akiongeza kuwa kila mtu ana wajibu wa kulinda mazingira kwa vitendo badala ya maneno.


Katika hatua nyingine, Bi. Rukia Zuberi aliwataka wataalamu wa mazingira pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuendelea kusimamia na kuimarisha programu za upandaji miti ndani ya Wilaya hiyo na kuhakikisha miti hiyo inayopandwa inatunzwa.


Pia alizitaka taasisi zote za umma na binafsi kuiga mfano huo kwa kupanda miti katika maeneo yao ya kazi na makazi yao kuhakikisha miti inatunzwa ipasavyo.


Hata hivyo, Bi. Rukia Zuberi alisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika juhudi hizi ili kuifanya Mwanga kuwa wilaya ya kijani na mfano wa uhifadhi bora wa mazingira nchini. 


Alitoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kuhakikisha inasimamia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo ili kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana kwa maendeleo endelevu ya eneo hilo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »