Na. Mwandishi Wetu , Dodoma
Wanawake kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Makao Makuu wameungana na wanawake wengine mkoani Dodoma kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2026, Jijini Dodoma
Katika kuadhimisha siku hii Wanawake hao wametoa msaada wa mahitaji mbalimbali katika Kituo cha Watoto Yatima cha Rahman kilichopo chang'ombe mkoani Dodoma, ili kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mahitaji hayo, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Bi. Subira Kaswaga, amesema kuwa mwaka 2026 mamlaka hiyo imeamua wanawake wa taasisi hiyo washiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo hufanyika tarehe 8 Machi kila mwaka.
Aidha, amebainisha kuwa Mamlaka ya Serikali Mtandao inathamini wanawake na inahakikisha wanashiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii ili kutoa motisha na hamasa kwa wanawake na wasichana kuwa na jitihada katika masomo yao pamoja na katika fani ya TEHAMA.
Bi.Kaswaga amebainisha kuwa kabla ya kutoa msaada huo, walitembelea baadhi ya vituo vya watoto yatima ili kubaini mahitaji yaliyopo na kuamua kuchagua vituo vyenye uhitaji mkubwa zaidi. Misaada hiyo ni vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, sukari, na viazi, pamoja na taulo za kike, mafuta, nguo, na viatu kwa ajili ya watoto wanaoishi katika kituo hicho. Baadhi ya vitu vimetolewa na mamlaka na vingine vimechangwa na watumishi wa taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Katibu wa Kituo cha Rahman, Abdallah Said, amewapongeza na kuwashukuru wanawake kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kutoa msaada huo kwa ajili ya kusaidia watoto wenye uhitaji, akibainisha kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka hasa katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Aidha, amebainisha kuwa kituo hicho kina jumla ya watoto 120 wanaopata huduma mbalimbali, huku kwa mujibu wa ustawi wa jamii, uwezo wa kituo kuwahifadhi watoto wanaolala ukiwa ni wa watoto wasio chini ya 46, ambapo watoto 74 hurudi katika kaya zao kwa bibi, babu, shangazi, au mjomba kutokana na uwezo mdogo wa kituo kuwahifadhi wote.
Maadhimisho ya mwaka 2026 yaliongozwa na kauli mbiu isemayo: “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi kuelekea Dira ya Taifa 2050.”




EmoticonEmoticon