Na.Alex Sonna-DODOMA
JUMLA ya wanawake 1916 wamefika katika viwanja vya Ofisi za Ardhi kufuatilia hati zao za ardhi na kupata huduma mbalimbali za masuala ya umiliki wa ardhi kupitia programu maalumu ya Samia Ardhi Kliniki inayofanyika Mkoa wa Dodoma.
Wanawake hao wamejitokeza kwa wingi kupata elimu kuhusu haki za umiliki wa ardhi, ushauri wa kitaalamu pamoja na kusaidiwa kukamilisha taratibu za kupata hatimiliki.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma Bi.Happiness Mtutwa,wakati akifunga kliniki maalum iitwayo Samia Ardhi Kliniki yenye Kauli Mbiu, Mwanamke; Haki Yako, Miliki Ardhi sasa.
"Katika kliniki hiyo, huduma mbalimbali zimetolewa ambapo hati 694 zimesajiliwa, hati 316 zimekabidhiwa kwa wanawake, migogoro 49 ya ardhi imetatuliwa, na wanawake 105 wamepata ushauri wa kisheria bila malipo. Mpango huo umeonesha mwitikio mkubwa wa wananchi hususan wanawake katika kufuatilia haki zao za umiliki wa ardhi."amesema Bi.Mtutwa
Amesema kuwa Kliniki hiyo imefanyika kuanzia Machi 2 hadi 7 Machi 2026, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, aliyoyatoa tarehe 12 Februari 2026 jijini Dodoma wakati akihitimisha Kliniki ya Ardhi. Lengo lake ni kuwapa wanawake fursa ya kupata huduma za ardhi kwa urahisi, sambamba na kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Katika kipindi hicho, viongozi wa mkoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule pamoja na Mkuu wa Wilaya Mhe. Jabir Shekimweri walitembelea kliniki hiyo kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za ardhi zinazowakabili wananchi.
Aidha amesema kuwa Taasisi mbalimbali zilishiriki kutoa huduma za ushauri na msaada wa kisheria, zikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
Hata hivyo Bi.Mtutwa amesema kuwa Programu ya Samia Ardhi Kliniki imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi kisheria na kupata haki zao, jambo linalochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa familia na jamii kwa ujumla.
Pia amewataka wanawake hao kwenda kuzitumia vizuri hati hizo ili ziweze kuwasaidia kiuchumi kwa kuweza kwenda nazo benki kwa ajili ya kukopa mikopo nafuu itakayowawezesha kuanzisha biashara na kuendelea kuimarisha uchumi wao.
Sambamba na hilo, Bi.Mtutwa pia amekabidhi hati miliki kwa baadhi ya wanawake waliofika katika kliniki hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma.
EmoticonEmoticon