TANZANIA NA GHANA KUIMARISHA USHIRIKIANO KIUCHUMI, AJIRA KWA VIJANA

March 02, 2026


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Ghana Mhe. John Dramani Mahama mara baada ya kuwasili katika Ikulu Ndogo ya Arusha tarehe 02 Machi, 2025. Rais wa Ghana Mhe. Mahama amewasili Mkoani Arusha kwa ajili ya Ziara ya Kikazi, ambapo anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Mwaka mpya wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, na Sherehe za kumbukizi ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mahakama hiyo mwaka 2006.

…………….

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mazungumzo ya pande mbili na Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mheshimiwa John Dramani Mahama, yaliyofanyika Ikulu jijini Arusha, yakilenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika masuala ya uchumi, ajira kwa vijana na maendeleo ya uchumi wa kidijitali.

Akizungumza kuhusu mazungumzo hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, amesema viongozi hao wamejadili kwa kina namna ya kuongeza thamani ya rasilimali za ndani ili kukuza uchumi wa mataifa yao badala ya kuendelea kuuza malighafi.

“Marais wamekubaliana kuwa wakati umefika kwa nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika uchakataji na kuongeza thamani ya mazao na rasilimali zao, hatua itakayoongeza mapato ya ndani na kuzalisha ajira kwa vijana,” amesema Machumu.

Kwa mujibu wa Machumu, Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, ameeleza uzoefu wa nchi yake katika kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kakao, akisisitiza umuhimu wa sera madhubuti za ndani zinazolenga kukuza uchakataji wa bidhaa hizo kabla ya kuzipeleka katika masoko ya kimataifa.

Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inaendelea kuharakisha mkakati wa uchumi wa viwanda, ikiwemo kuongeza thamani ya mazao ya kimkakati kama pamba na kuimarisha uchakataji wa madini, huku akibainisha kuwa uzoefu wa Ghana ni muhimu katika safari hiyo.

Machumu amesema suala la ajira kwa vijana limepewa kipaumbele katika mazungumzo hayo, ambapo viongozi hao wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika maendeleo ya ujuzi, ubunifu na ujasiriamali ili kuweka mazingira bora ya uwekezaji yatakayozalisha ajira endelevu kwa vijana.

Katika eneo la uchumi wa kidijitali, Rais Dkt. Samia amesisitiza dhamira ya Tanzania ya kuimarisha mifumo ya fedha za kidijitali na usalama wa mitandao kama sehemu ya mkakati wa kujenga uchumi shindani na jumuishi. Ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA na kukuza ubunifu wa vijana, huku akitaja sekta ya teknolojia ya fedha ya Ghana kama eneo muhimu la kujifunza na kushirikiana.

Aidha, viongozi hao wamepongeza hatua ya kuimarishwa kwa safari za Shirika la Ndege la Air Tanzania Company Limited> (ATCL) kati ya Tanzania na Ghana, wakisema hatua hiyo itarahisisha biashara, utalii na mwingiliano wa watu, na kuchochea biashara ndani ya Bara la Afrika.

Rais wa Ghana yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja. Leo, tarehe 02 Machi, 2026, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama na Maadhimisho ya Miaka 20 ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yenye makao makuu jijini Arusha.



R

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Ghana Mhe. John Dramani Mahama, katika Ikulu Ndogo ya Arusha tarehe 02 Machi, 2025. Rais wa Ghana Mhe. Mahama amewasili Mkoani Arusha kwa ajili ya Ziara ya Kikazi, ambapo anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Mwaka mpya wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, na Sherehe za kumbukizi ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mahakama hiyo mwaka 2006.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Jamhuri ya Ghana Mhe. John Dramani Mahama mara baada ya mazungumzo yao katika Ikulu Ndogo ya Arusha, tarehe 02 Machi, 2025.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »