SERIKALI YASISITIZA ULINZI WA AJIRA NA UKUAJI WA UCHUMI KUPITIA VIWANDA

March 02, 2026

Serikali kuendelea kuweka mazingira salama kwa wenye Viwanda vinavyofanya kazi na kutatua changamoto kwa wakati ili kuendelea kulinda ajira za Watanzania na kuongeza mzunguko wa fedha kwa jamii na wananchi kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo (Mb) wakati wa ziara ya kikazi Machi 2, 2026 mkoani Morogoro.

Londo amemshauri Katibu Tawala mkoani Morogoro kuweka utaratibu kwa mikopo ya asilimia 10 kuwafikia walengwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda vidogo (SIDO) ili kuleta maana ya utoaji wa mikopo kwa jamii nchini.

Londo ametembelea viwanda vinne katika Manispaa ya Morogoro ikiwemo SIDO, Mkwawa, Cotex na Mazava katika ziara yake ya siku moja mkoani hapa.

Pia amesema ikiwa wajasiliamali hao watapata mikopo wakiwa hapo ambako wamezungukwa na aina mbalimbali za ujasiriamali itawasaidia kupata namna ya kujengwa na kuwa wajasiriamali wazuri na hivyo kuwa na uhakika wa kurejesha mikopo hiyo.

Uwepo wa gundi inayozalishwa kwenye viwanda hivyo vidogo vilivyopo kwenye eneo la viwanda SIDO Morogoro ambapo ameiomba serikali ya mkoa kusimamia uzalishaji huo na kufanya masoko makubwa ya gundi kuanzia ndani ya mkoa na kisha nje ya mkoa Taifa hadi nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji anasema wanajipanga kuhakikisha wanaboresha eneo la viwanda la SIDO Morogoro ili kufanya wajasiriamali kulitumia kama kongani la viwanda na kuleta maana

Hata hivyo, Meneja wa SIDO Morogoro, Bi.Joan Nangawe anasema wametengeneza ajira zaidi ya 115 baada ya kutoa elimu, kuwakusanya wajasiriamali kwenye eneo la viwanda na kutoa mikopo ya shilingi Milioni 62.5.

Anasema katika siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan jumla ya wajasiriamali ambao ni vijana wanatarajia kupata mikopo ya shilingi Milioni 250 kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.

Mmoja wa wajasiriamali anayetengeneza Gundi kwenye eneo la viwanda SIDO Marry Hassan anasema licha ya kuwa na uhakika wa soko la ndani kwa mikoa ya Morogoro na Dar es salaam lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa masoko ya nje ambayo yanaweza kuwapa nafasi kubwa katika kuongeza uzalishaji na kukua kiuchumi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »