
Ofisi ya BAKWATA Mkoa wa Singida, kupitia Sheikh wa Mkoa huo Issa Bin Nassoro, imezipongeza taasisi za Ramadhan Charity Programme2026, inayoongozwa na Ndugu Ahmed Misanga pamoja na Taasisi ya JAI Tanzania kwa kutoa sadaka katika Gereza la Manispaa ya Singida, misikiti pamoja na vituo vya watoto yatima.
Sheikh Issa amesema hayo leo wakati wa ziara yake ya kutembelea wafungwa katika Gereza la Manispaa ya Singida, ambapo pia walitoa sadaka ya Iftar kwa wafungwa ili waweze kupata futari pamoja na daku katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Sadaka hizo zimetolewa na taasisi za Ramadhan Charity Programme 2026 pamoja na JAI Tanzania.
Katika hotuba yake, Sheikh Issa aliwaomba watu mbalimbali katika jamii kuwajali watu wenye mahitaji na masikini, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni jambo linalompendeza Mungu. Aliongeza kuwa hata mitume waliwahudumia na kuwasaidia watu masikini na wenye uhitaji.
Aidha, Sheikh wa Mkoa alitoa salamu kutoka kwa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir bin Ally, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwajali watu wenye mahitaji maalum, wakiwemo wafungwa na makundi mengine yenye uhitaji katika jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ramadhan Charity Programme 2026, Ndugu Ahmed Misanga, amesema kuwa utoaji wa sadaka ya Iftar kwa watu wenye mahitaji ni utaratibu wao wa kila mwaka, hususan katika magereza na makundi mengine ya jamii. Amesema kuwa wamekuwa wakifanya shughuli hiyo kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Misanga alisisitiza kuwa watu waliopo magerezani wanahitaji huruma na faraja kutoka kwa jamii ili kuwapa moyo na kuwasaidia kumkaribia Mungu, ili wanaporudi uraiani wawe watu wema wenye hofu ya Mungu na mchango chanya kwa jamii.
Katika msaada huo, Ramadhan Charity Programme 2026 kwa kushirikiana na JAI Tanzania walitoa sadaka ya Iftar iliyojumuisha boksi la tende, sukari, tambi, mchele, ngano, juisi pamoja na taulo za kike kwa ajili ya wafungwa wanawake katika gereza hilo.
Naye Kaimu Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Singida, Ndugu Amini Mjenza, amesema amefurahishwa na taasisi ya Ramadhan Charity chini ya uongozi wa Ahmed Misanga kwa kuwapatia sadaka ya Iftar, akieleza kuwa msaada huo utawasaidia sana wafungwa waliopo gerezani.
“Tutaitumia sadaka hii ya Iftar kama mlivyokusudia, na tunamuomba Mungu awalipie pale mlipotoa kwa ajili ya wafungwa wote, wanawake na wanaume,” amesema.
Katika tukio hilo, washiriki pia walipata nafasi ya kuliombea Taifa pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taasisi ya Ramadhan Charity Programme 2026 imewataka Watanzania kutumia mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kuwa wamoja, kusaidiana na kufanya kazi kwa pamoja katika kuwasaidia wenye mahitaji katika jamii.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


EmoticonEmoticon