DID TANZANIA KUTOA ELIMU YA UTUNZAJI MAZINGIRA ROMBO KWA KUTUMIA SANAA YA MAJUKWAANI

March 31, 2026

 




Na. Mwandishi Wetu,


DIVERSITY Initiatives for Development Tanzania (DID TANZANIA) ambao ni waratibu wa mradi wa Sauti za Mabonde "Voices of Valley" uliojikita kutoa elimu ya utunzaji wa Mazingira Wilayani Rombo wanatarajia kufikia Jamii kwa kutumia Sanaa ya majukwaani.


Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa DID Tanzania, Bw. Optatus Nestory Mbararia ambaye ni mratibu mkuu wa mradi amesema kuwa, utafiti wa awali wamebaini uharibifu mkubwa wa Mazingira ikiwemo eneo la chanzo cha maji cha Kamdawi na bonde la Tarakea, unaotokana na shughuli za Kijamii kama uchimbaji mchanga, kubonda kokokoto, ukataji wa miti na Kilimo kisicho rasmi pembezoni mwa vyanzo vya maji.

"Kwa sasa tupo hatua ya mwisho kwa Vijana Wasanii wakifanya mazoezi ya onesho lao kwa njia ya sanaa za jukwaani.


Watafanya maonesho kadhaa ambayo ni ya wazi jukwaani, kufikisha ujumbe." Amesema Optatus Mbararia.

Mradi ni wa mwaka mmoja, ambapo unaenda kutoa elimu kwa Jamii juu ya utunzaji wa Mazingira hususani vyanzo hivyo vya maji na mito mbalimbali Wilayani Rombo, Mkoani Kilimanjaro.


Aidha, amebainisha kuwa, mbali ya utoaji elimu kwa njia ya  Sanaa za majukwaani, Pia watakuwa na shughuli za upandaji miti kama utunzaji wa Mazingira, ambapo miti zaidi ya 1,000 itapandwa katika chanzo cha maji kamdawi na bonde la Mto Tarakea.

"Mradi wetu huu pia tunatarajia kushirikiana na wadau muhimu ikiwemo Halmashauri ya Rombo kupanda miti.


Lakini pia mijadala ya kijamii na Wananchi watatoa maoni yao." Amesema Bw. Optatus Nestory Mbararia.

Kwa Upande wao baadhi ya Wasanii Vijana wamebainisha kuwa wapo tayari na wamejiandaa vyema kufikisha elimu ya utunzaji mazingira kwa njia ya Sanaa za majukwaani 

Dumey Aloys Kijwiti msanii wa sanaa maagizo asema kupitia sanaa ujumbe utafika kwa haraka kwa Jamii.


"Naamini  Sanaa ni njia rahisi kufikisha ujumbe kwa Jamii, ni kitu rahisi zaidi kuliko chochote.


Sanaa ni njia rahisi ya kutatua na kuchanganua na kuleta majibu katika Jamii.


Kwa kupitia mradi wa voices of valley, nikiwa kama mratibu wa maigizo ya jukwaani, naamini na wenzangu tunaendelea vyema kufikisha ujumbe kwa Wananchi.


Sanaa kwa maendeleo Ina aina zake, kwa maana Sanaa Ina hatua zaidi ya Saba, na sie mwisho wa siku tunaenda kufanya Sanaa kwa  maendeleo.


Naamini Jamii itatupokea vizuri kwani tunaenda kuwapa mawazo mapya na kuonesha mambo ambao hayatakiwi kwa Jamii, na kulinda mazingira." Amesema Dumey.


Mradi huo ni program ya Vijana Artwork (Vijanam @rtwork) unasimamiwa na CDEA na Goethe Institut kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).



Mwisho.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »