Na Oscar Assenga, Handeni
MKUU wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, amesema uwepo wa taasisi za kifedha, ikiwemo Benki ya NMB, ni nyenzo muhimu katika kuchochea na kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia sekta mbalimbali kama kilimo, mifugo na biashara ndogondogo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutilia mkazo juhudi za kuimarisha uchumi wa wananchi wa vijijini ili waweze kujikwamua kiuchumi na kimaendeleo.
Nyamwese alitoa kauli hiyo leo wakati wa tamasha la “NMB Kijiji Day” lililoandaliwa na Benki ya NMB wilayani Handeni, likihusisha matembezi, mbio fupi na mazoezi, kwa lengo la kuwakutanisha wananchi na kuwahamasisha kushiriki shughuli za maendeleo.
Alisema uwepo wa benki hiyo katika tamasha hilo haujalenga kutangaza huduma zake pekee, bali pia kutoa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo upimaji wa afya na uchangiaji wa damu, jambo ambalo lina manufaa makubwa kwa jamii.
“Ninawahimiza wananchi wa Handeni kutumia fursa hii kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha, kufungua akaunti na kujifunza namna bora ya kusimamia mapato yao. Ni muhimu pia kuhakikisha mikopo inayopatikana inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta tija kwa familia na jamii kwa ujumla,” alisema Nyamwese.
Aidha, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan waliopo maeneo ya pembezoni kupitia mtandao mpana wa matawi na mawakala.
Awali, akizungumza katika tamasha hilo, Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi wa Benki ya NMB Makao Makuu, Donatus Richard, alisema “NMB Kijiji Day” ni jukwaa muhimu la kushirikiana na jamii kupitia utoaji wa elimu ya kifedha na huduma za kibenki.
Alisema kupitia tamasha hilo, benki hiyo hutoa elimu ya masuala ya fedha, kufungua akaunti kwa wananchi na kuimarisha mshikamano wa kijamii, sambamba na kuhamasisha afya na ustawi kupitia michezo na burudani.
Donatus alibainisha kuwa hapo awali huduma nyingi za kibenki zilikuwa zinapatikana zaidi mijini, lakini kuanzia mwaka 2024 benki hiyo ilianza mkakati wa kupeleka huduma hizo vijijini.
“Kwa sasa tuna matawi zaidi ya 248 nchini kote, na hata maeneo yasiyo na matawi tunahakikisha huduma zinapatikana kupitia mawakala. Tumeweza kufikia zaidi ya vijiji 3,000 tangu mwaka 2024 ambavyo hapo awali havikuwa na huduma za kibenki,” alisema.
Aliongeza kuwa juhudi hizo zimeongeza idadi ya wateja, ambapo zaidi ya akaunti milioni mbili zimefunguliwa kuanzia mwaka 2024 hadi Januari mwaka huu.
Kwa mwaka 2026, alisema benki hiyo imejipanga kufikisha huduma za kibenki katika vijiji vingine 2,000 ambavyo bado havijafikiwa, sambamba na kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii kama michezo na upandaji miti ili kulinda mazingira.
Aidha, alisema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira, ikiwemo kuhimiza matumizi ya nishati safi badala ya mkaa.
“Benki yetu inatambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira na tunatambulika kimataifa kwa uwajibikaji wa kijamii. Fedha za wateja wetu ziko salama na wanapata huduma bora kwa wakati,” alisema.
Alibainisha kuwa mwaka 2026 benki hiyo imetambuliwa kwa ubora katika masuala ya uendelevu nchini, ikiwa na zaidi ya matawi 248, mashine za ATM zaidi ya 700, mawakala 73,000 na wateja zaidi ya milioni 10.
Mwisho, alitoa wito kwa wananchi ambao bado hawajafungua akaunti kufanya hivyo ili waweze kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.
Mwisho.

EmoticonEmoticon