WAZIRI NDEJEMBI -BOMBA LA GESI NTORYA-MADIMBA LIKAMILIKE IFIKAPO SEPTEMBA 2026

February 27, 2026


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kumsimamia kikamilifu Mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka eneo la ugunduzi la Ntorya hadi Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba ili kuhakikisha unakamilika ifikapo Septemba 2026

Amesema hayo, leo tarehe 27 Februari 2026 mkoani Mtwara mara baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa bomba la gesi asilia Ntorya–Madimba ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 35 akieleza kuwa mradi huo utachangia kuongeza matumizi ya gesi asilia na kuchochea ukuaji wa uchumi

“Tumeweka ‘taget’ ya mwezi wa tisa kuhakikisha visima hivi vinazalisha gesi na kuunga kwenye bomba kuu la Madimba, ikifika muda huo kusiwe na hadisi nyingine, ili haya yasitokee tunahitaji usimamizi wa hali ya juu kuhakikisha TPDC mnakuwa site muda wote, Watanzania wanataka wanataka kuona maendeleo,” amesisitiza Ndejembi

Aidha, Ndejembi amewataka wataalamu wa TPDC kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa ubora na kwa kuzingatia muda uliokubaliwa kwenye mkataba huku akibainisha kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa sekta ya gesi kwa kuongeza uzalishaji wa umeme kuvutia uwekezaji na kukuza viwanda vitakavyozalisha ajira kwa Watanzania

Ameihimiza TPDC kuongeza kasi ya utafutaji na uendelezaji wa visima vipya ili kuhakikisha upatikanaji wa gesi ya kutosha hususan ikizingatiwa kuwa miundombinu ya usafirishaji tayari ipo nchini pamoja na kutekeleza kikamilifu miradi ya uwajibikaji kwa jamii katika maeneo ya mradi kwa kushirikiana na wananchi kutatua changamoto kama ujenzi wa vyumba vya madarasa uchimbaji wa visima vya maji na miradi mingine kulingana na mahitaji ya eneo husika

Vilevile, Waziri Ndejembi amesema Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imelenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya gesi asilia hatua itakayowezesha kufikiwa kwa lengo la kuzalisha megawati 8000 za umeme ifikapo mwaka 2030

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Dkt. James Mataragio amesema kitalu cha Ntorya kitaongeza upatikanaji wa gesi asilia huku akibainisha kuwa mahitaji ya gesi hiyo yanaongezeka kila siku na wawekezaji wa viwanda wamekuwa wakiwasilisha maombi ya gesi hiyo

Mradi wa bomba la kusafirisha gesi asilia ghafi kutoka kitalu cha Ntorya ulisainiwa tarehe 3 Julai 2025 kati ya TPDC na mkandarasi wa kampuni za China Petroleum Pipeline Engineering Co. Ltd. na China Petroleum Technology & Development Corporation kwa thamani ya Dola za Marekani Milioni 46.8 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Septemba 2026


.





Share this

Related Posts

Previous
Next Post »