NCHI ZA SAPP ZAKUTANA KUHAMASISHA MATUMIZI BORA YA NISHATI

February 05, 2026


📍TANESCO kuendesha kampeni ya matumizi bora ya umeme


📍Ni katika kutekeleza kwa kasi Mkakati wa Wizara ya Nishati wa mwaka 2024–2034


Na Mwandiahi Wetu – Zanzibar


Wajumbe wa Nchi Wanachama wa Ujumuiya ya Ushirikiano wa Umeme wa Kusini mwa Afrika (SAPP), zinazotoka katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wakishirikisha makampuni ya umeme zaidi ya 16 yanayojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa umeme, wamekutana Zanzibar kujadili na kuhimiza matumizi bora ya nishati ya umeme.


Mkutano huo wa siku mbili ulioanza tarehe 04 Februari 2026 unalenga kuhakikisha nishati ya umeme inayopatikana katika nchi wanachama inatumika kwa ufanisi na ubora zaidi, ikihusisha matumizi ya umeme kwa kiasi kidogo huku uzalishaji ukiendelea kuongezeka, ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa nchi husika.

Akizungumza katika mahojiano na waandishi wa habari, Meneja Tafiti wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Samweli Kessy, alisema kuwa licha ya gharama kubwa za uzalishaji wa umeme, mashirika ya umeme huuza umeme kwa bei nafuu kwa wananchi, hivyo elimu ya matumizi bora ya umeme ni muhimu katika kuokoa nishati na kuongeza mapato ya taifa kupitia uuzaji wa umeme nje ya nchi.

Aidha, Mhandisi Kessy aliongeza kuwa matumizi bora ya umeme husaidia kupunguza gharama za uzalishaji na wakati huo huo kuchangia katika uhifadhi wa mazingira.


Alisema kuwa kwa upande wa Tanzania, Wizara ya Nishati imeandaa Mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati wa mwaka 2024 hadi 2034, unaolenga kuhakikisha wananchi wote wanapatiwa elimu ya matumizi bora ya umeme, hatua itakayopunguza gharama za maisha na kuongeza ufanisi wa matumizi ya huduma ya umeme.

Aliongeza kuwa, kupitia Mkakati wa Mawasiliano wa TANESCO, shirika litaendelea kutumia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, redio, televisheni, magazeti pamoja na mikutano ya ana kwa ana ili kuwafikia wananchi na wadau katika ngazi zote.

Mhandisi Kessy alibainisha kuwa mpango huo utahusisha wateja wote, kuanzia wateja wakubwa, wa kati hadi wadogo katika ngazi za mikoa, wilaya, kata na vijiji kote nchini.


Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kukamilika tarehe 05 Februari 2026.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »