📌Rais Samia apewa shurkani kwa kuendelea kuiwezesha TANESCO
📌Menejimenti yaahidi kuboresha huduma ya umeme kwa wananchi
*Na Amanda Tagame Dodoma*
Watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wamehimizwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuliwezesha Shirika kutimiza malengo yake na kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia umeme wa uhakika na wa kutosha kwa maendeleo ya Shirika na Taifa.
Wito huo umetolewa wakati wa kufungwa kwa Kikao cha 55 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TANESCO kilichofanyika jijini Dodoma, ambapo Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Mheshimiwa Balozi Zuhura Bundala, alimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo tarehe 24 Januari, 2026.
“Niwaombe muendelee kuchapa kazi kila mmoja katika eneo lake kama ilivyo siku zote, ili Shirika letu lizidi kuimarika kiutendaji na kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu,” alisema Balozi Bundala.
Aidha, alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuliwezesha Shirika kutekeleza majukumu yake kwa kutoa fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati nchini yenye lengo la kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Napenda kutumia nafasi hii kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha Shirika letu kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya umeme inayolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini,” aliongeza.
Vilevile, ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti kwa usimamizi mzuri wa maslahi ya wafanyakazi, hali iliyopelekea kuboreshwa kwa mishahara na motisha kwa lengo la kuongeza ari ya kazi.
Aidha,amewataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya Shirika na Taifa, pamoja na kuzingatia misingi ya sheria na maadili ya utumishi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, alimshukuru Mwenyekiti wa Bodi kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa na Bodi ya Wakurugenzi katika kusimamia rasilimali na maendeleo ya Shirika, hali inayoliwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Naishukuru kwa dhati Bodi ya Wakurugenzi kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa Menejimenti katika kusimamia masuala ya Shirika, ikiwemo maslahi ya wafanyakazi. Tunaahidi kuendelea kusimamia mipango na mikakati ya Shirika kwa kuongeza mapato na kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Bw. Twange.
Kikao hicho kilichowakutanisha uongozi wa shirika,wawakilishi wa wafanyakazi pamoja na Chama cha Wafanyakazi (TUICO) kilianza mapema wiki hii na kimeazimia kuendelea kuimarisha utendaji kazi na ushirikiano kwa ustawi wa Shirika.






EmoticonEmoticon