KIONGOZI MPYA ASIMIKWA- HIFADHI YA TAIFA RUAHA,AHAIDI KUENDELEZA MAZURI YOTE YALIYOANZISHWA

January 03, 2026


Leo Januari 02, 2026 yamefanyika makabidhiano kwa uongozi mpya wa Mkuu Hifadhi ya Taifa Ruaha kutoka mikononi mwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Abeli Mtui kwenda kwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Emmanuel Moirana, makabidhiano yaliyofanyika Makao Makuu ya Hifadhi hiyo yaliyopo Msembe takribani kilometa 130 kutokea mjini Iringa.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kamishna Mtui aliwashukuru Maafisa na Askari wa hifadhi hiyo kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati wa uongozi wake.


Aidha, Kamishna Mtui Alisisitiza kuwa ushirikiano huo ndio umekuwa msingi mkubwa wa mafanikio katika sekta ya utalii, ulinzi wa maliasili ambao umeimarika sanjali na uboreshaji wa miundombinu ya malazi kwa wageni na viwanja vya ndege.


Kwa upande wake Kamishna Moirana aliahidi kuendeleza ushirikiano, nidhamu na uwajibikaji, huku akibainisha kuwa atafanya kazi kwa ukaribu na menejimenti na watumishi wa hifadhi hiyo ili kuimarisha uhifadhi na usimamizi endelevu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha.


Kabla ya kukabidhiwa Hifadhi ya Taifa Ruaha leo, Kamishna Moirana alikuwa ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi, na aliyekuwa Mkuu wa hifadhi hiyo, Kamishna Dkt. Abel Mtui anaenda Makao Makuu ya Shirika yaliyopo jijini Arusha kuwa Mkuu wa Kitengo cha GIS (Geographic Information System).

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »