WIZARA YA NISHATI YATAMBUA MCHANGO WA VYOMBO VYA HABARI KATIKA SEKTA YA NISHATI

January 03, 2026


📌*Yawashukuru Waandishi wa Habari kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na kwa wakati*


📌*Yaahidi Kuimarisha Mawasiliano ya Kimkakati Mwaka 2026*


Wizara ya Nishati imepongeza mchango mkubwa wa vyombo vya habari nchini kwa kuwa washirika wa karibu na nguzo muhimu katika kuhakikisha Watanzania wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu Sekta ya Nishati.


Akizungumza Jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Bi. Neema Mbuja, amesema ushirikiano uliopo kati ya Wizara na vyombo vya habari umeiwezesha Serikali kufikisha kwa ufanisi taarifa za miradi, mafanikio na mwelekeo wa sekta ya nishati kwa wananchi katika mwaka 2025.


Bi. Mbuja amesema waandishi wa habari na wahariri wamekuwa daraja muhimu kati ya Serikali na wananchi, kwa kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu masuala yanayohusu umeme, mafuta, gesi asilia pamoja na nishati safi ya kupikia—sekta ambazo zina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi.


Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano huo, Wizara imefanikiwa kuongeza uelewa wa umma kuhusu utekelezaji wa miradi mikubwa ya nishati nchini, hali iliyosaidia kuimarisha uwazi, uwajibikaji na imani ya wananchi katika jitihada za Serikali za kuleta maendeleo endelevu.


“Vyombo vya habari vimekuwa mshirika wetu wa karibu katika kufikisha ujumbe wa Wizara kwa wananchi. Kupitia kazi za Waandishi wa habari, jamii imepata uelewa mpana kuhusu masuala ya nishati yanayogusa moja kwa moja maisha ya kila siku,” amesema Bi. Mbuja


Akizungumzia mwelekeo wa mwaka 2026, Bi. Mbuja amesema Wizara ya Nishati imejipanga kuimarisha zaidi mawasiliano ya kimkakati kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na vyombo vya habari, ili kuhakikisha taarifa zote zinazotolewa zinakuwa sahihi, zenye tija na zinamfikia mwananchi kwa ufanisi zaidi.


“Ninapenda kuwashukuru sana wadau wetu wa vyombo vya habari, wahariri pamoja na waandishi wa habari kwa kazi kubwa mliyoifanya mwaka 2025 ya kuitangaza Wizara ya Nishati. Mwaka 2026 tunaenda kuimarisha zaidi mawasiliano ya kimkakati ili kuhakikisha Watanzania wanapata taarifa sahihi kutoka kwetu, kwa kuwa Wizara ya Nishati ni wizara inayochochea ukuaji wa uchumi wa nchi yetu,” Amesisitiza Bi.Mbuja


#NishatiTupoKazini

#Tunasikiliza

#NchiYetuKwanza

#TunasongaMbelePamoja

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »