HESHIMA KAMBI YA TBN:VERONICA MREMBA AINGIA JOPO LA MDAHALO MKUTANO MKUU WA DUNIA WA WAANDISHI WA SAYANSI

December 01, 2025

PRETORIA, AFRIKA KUSINI


Kilele cha utambuzi wa uandishi wa habari za kidijitali nchini Tanzania kimethibitishwa baada ya Bi. Veronica Mrema, Mwanzilishi wa chombo cha habari cha M24 TANZANIA MEDIA na mwanachama mahiri wa Tanzania Bloggers Network (TBN), kuingia rasmi kwenye jopo la mdahalo katika Mkutano wa 13 wa Kimataifa wa Waandishi wa Habari za Sayansi (WCSJ2025) unaofanyika jijini Pretoria.


Hili si tu fahari kwa Mrema binafsi, bali ni heshima kubwa kwa TBN na tasnia nzima ya habari nchini, ikionesha kuwa kazi ya uandishi wa kidijitali inatambulika katika majukwaa makuu duniani.


Mrema yuko Afrika Kusini kuhudhuria mkutano huo mkuu unaotarajiwa kudumu hadi Desemba 5, 2025, baada ya kukabidhiwa udhamini maalum wa safari (Travel Grant) na Wizara ya Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu ya Afrika Kusini (DSTI). Udhamini huu ulikuja kama matunda ya utambuzi wa utendaji wake wa kipekee katika uandishi wa habari za kisayansi na afya, akibainishwa kuwa miongoni mwa wachache barani Afrika waliochaguliwa kwa heshima hiyo. Uwepo wake kwenye jopo la mdahalo unampa fursa adhimu ya kushiriki moja kwa moja katika kuunda mwelekeo wa mustakabali wa habari za sayansi duniani.


Akiwa anahutubia jukwaa la WCSJ2025 ambalo linakutanisha waandishi, watafiti, na wataalamu mashuhuri kutoka kote duniani, Veronica Mrema anatarajiwa kusisitiza kuwa tasnia ya habari za sayansi na afya barani Afrika inakua kwa kasi na kwa hivyo inahitaji sasa zaidi ya wakati mwingine uandishi wa weledi wa hali ya juu, ubunifu, na ushahidi wa ki-sayansi ili kufikisha ujumbe sahihi na wa kuaminika kwa jamii.


Lengo lake kuu ni kuhakikisha uelewa sahihi wa sayansi unakuza maamuzi yanayoleta maendeleo, huku akitumia uzoefu wake kama kiongozi, ikiwemo nafasi yake kama Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC) na Afisa Habari wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Selimundu Tanzania (SCDPCT), kutetea uandishi wenye tija.


Kutambulika huku kwa Mwanachama wa TBN kunaimarisha nafasi ya Tanzania katika uwanja wa uandishi wa habari za kisasa, kuashiria kwamba mchango wake katika upashanaji habari ni wa kiwango cha kimataifa.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »