WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA YAWA FURSA YA TTCL KUKUSANYA MREJESHO WA WATEJA

October 10, 2025


Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limehitimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025 likiwa na azma ya kuendelea kuboresha ubora wa huduma zake, kupanua miundombinu ya mawasiliano na kusikiliza kwa karibu maoni ya wateja wake kote nchini.

Akizungumza katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 10 Oktoba 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Ndg. Humphrey Ngowi, amesema wiki hiyo imekuwa jukwaa muhimu la kujifunza, kutathmini mafanikio na kupanga maboresho ya huduma kulingana na mahitaji halisi ya wateja.

“Wiki hii imetupa fursa ya kukusanya mrejesho kutoka kwa wateja, kuainisha mapungufu na kuandaa maboresho yatakayoboresha huduma zetu zaidi. TTCL itaendelea kutoa huduma bora, za kuaminika na zenye ubora wa hali ya juu,” amesema Ngowi.

Amesema TTCL, kama nguzo ya mawasiliano nchini, imeendelea kufanya maboresho makubwa kupitia miradi ya kimkakati ikiwemo upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ujenzi wa minara mipya vijijini na mijini, pamoja na kuimarisha mifumo ya mawasiliano ya kidijitali.

Ngowi ameongeza kuwa, katika dunia ya sasa ya ushindani wa kiteknolojia, TTCL imeweka mkakati madhubuti wa kuboresha huduma kwa wateja kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuongeza thamani katika kila huduma inayotolewa.

“Wateja wetu ndio sababu kuu ya sisi kuwepo. Kaulimbiu ya mwaka huu ‘Mission Possible’ si maneno tu, bali ni uhalisia tunaouishi kila siku katika kuwahudumia Watanzania,” amesisitiza.

Akitoa shukrani kwa watumishi wa TTCL na wateja walioshiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo, Ngowi alisema mafanikio yaliyopatikana mwaka huu ni matokeo ya kazi ya pamoja na moyo wa kujituma wa wafanyakazi wa shirika hilo.

Amewahakikishia Watanzania kwamba TTCL itaendelea kuwa kinara wa mawasiliano nchini, ikitoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa na kuhakikisha kila mteja anapata huduma yenye thamani na ubora unaostahili.

Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa duniani kote kila mwezi Oktoba kwa lengo la kutambua mchango wa wateja na kuimarisha uhusiano kati ya watoa huduma na wateja wao.














Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »