-Waeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wake
-Wasema umeibua fursa lukuki
Wakazi wa vitongoji vya Chihanga, Mpilipili, Mkwedu na Majengo Wilayani Newala Mkoani Mtwara wameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kufikisha umeme katika vitongoji hivyo.
Wametoa pongezi hizo Oktoba 19, 2025 kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni maalum ya kuhamasisha wananchi vitongojini kujiunga na huduma ya umeme inayoratibiwa na REA.
“Tunashukuru kufikishiwa umeme kitongojini hapa, maisha yetu kwa sasa yameboreshwa ukilinganisha na hali ilivyokuwa hapo kabla ya kufikishiwa huduma hii muhimu ya umeme,” alisema Litehu Rashid Mkazi wa Kitongoji cha Chihanga
Kwa upande wake Bi. Skina Kunkatila Mkazi wa Kitongoji cha Mpilipili alifafanua namna ambavyo umeme umekuwa mkombozi katika maisha yake na alieleza adha mbalimbali zilizokuwepo kabla ya kufikishiwa nishati ya umeme na hali ilivyo sasa ambapo alisema kwa sasa kitongoji hakina tofauti na mji kwani huduma muhimu zote zinazohitaji umeme zinapatikana.
Naye Mwanahamisi Hassan maarufu kama Binti Nankomwanga Mkazi wa kitongoji cha Majengo alisema hapo zamani iliwalazimu kutembea umbali mrefu kusaga mahindi jambo ambalo kwa sasa halipo tena.
“Kitongoji chetu kimenoga, mwaka wa nyuma tulikuwa tunasafiri kwenda kusaga mahindi lakini sasa hivi kijiji kimechangamka, wananchi wanafanya biashara ya vinywaji baridi na suala la afya liko vizuri vifaa tiba vinavyotumia umeme vinafanya kazi,” alisema Binti Nankomwanga.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vitongoji hivyo, Msimamizi wa miradi ya REA Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Daniel Mwandupe alisema lengo la kampeni hiyo ya uhamasishaji ni kutoa elimu kwa wananchi ili kuelewa hatua za utekelezaji wa mradi unaoendelea wa kusambaza umeme, elimu ya kuomba kuunganishiwa umeme kwa kaya ambazo bado hazijafikiwa sambamba na kujadili changamoto zinazowakabili wananchi kwenye sekta ya umeme ili kupata ufumbuzi wa pamoja.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka REA, Jaina Msuya alitoa wito kwa wananchi ambao hawajaunganishwa na huduma ya umeme kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa kwa gharama ya shilingi 27,000 pekee.
Msuya aliwasisitiza kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya umeme ili waendelee kunufaika na kupiga hatua zaidi kimaendeleo hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu hiyo kwa lengo la kuwakwamua kimaendeleo wananchi wake.
EmoticonEmoticon