Na Hamida Kamchalla, TANGA.
KUFUATIA kero ya mikopo ya kausha damu kuwaandama wanawake wengi wanaojaribu kujikwamua kiuchumi katika Mkoa wa Tanga, Taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa riba nafuu zinahitajika jijini humo ili kuwanusuru wanawake hao.
Mgombea Ubunge Jimbo la Tanga mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (Ccm), Kasimu Mbaraka ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wa kampeni zake katika kata ya Mzingani jijini Tanga na kuwaahidi wananchi jimboni humo kuwaondolea kero hiyo ambayo imekuwa ikiwadhalilisha na kuwakosesha amani wanawake.
"Nahitaji kualika Taasisi za fedha zije mkoani Tanga ili kuja kutoa mikopo isiyo na riba kwa wananchi na kuondokana na mikopo ya kausha damu inayodhalilisha na kuwatesa wakina mama" alisema
Naye mgombea udiwani wa kata ya Mzingani Hamza Bwanga ametoa ahadi zake kwa wananchi hao kuwawezesha kupata mikopo kwa kuunda vikundi na kupewa elimu juu ya mikopo hiyo,, pamoja na kutafuta kero zilizopo mara tu watakapompa ridhaa ya kuongoza.
"Fedha zile zimewekwa kwa ajili ya wananchi wajasiriamali, vijana asilimia 4, wakina mama asilimia 4 na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu, mbali ya kutoa elimu kwa wananchi, nitakapokuwa kule halmashauri nitahakikisha naweka kipaumbele kwa vikundi vyote vya kata ya Mzingani vinapatiwa mikopo ile" amesema.
Hata hivyo wagombea hao wamesema ahadi hizo zipo nje ya ilani ya uchaguzi ya Chama hicho ya mwaka 2025/30 huku wakieleza mafanikio makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dr. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni pamoja na kumuombea kura za ndiyo ifikapo Octoba 29 kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.





EmoticonEmoticon