Na Yohana Kidaga- Nyakipande, Rufiji
Mgombea wa Ubunge jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kumchagua tena katika kipindi atahakikisha anaiomba Serikali iweze kusogeza zaidi huduma za afya ili kuboresha maisha ya wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kukiombea kura Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu kwa ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani katika Kijiji cha Nyakipande kata ya Chumbi jimboni Rufiji, Mhe. Mchengerwa amesema pamoja na kwamba tayari CCM kimefanya mambo makubwa kwenye huduma za jamii lakini bado atgahakikisha wananchi wa kata Chumbi wanajengewa kituo cha kisasa cha afya.
Amefafanua kuwa katika kipindi chake alipokea jimbo ikiwa baadhi ya maeneo wananchi wakitembea zaidi ya kilomita 70 kutafuta huduma za afya kwenye zahanati na vituo vya afya lakini hali ya sasa imebadilika.
“Ndugu zangu ni vizuri tuseme ukweli tulikotoka ni mbali, huduma nyingi za jamii kwa maana ya huduma ya afya, elimu hata miundombinu ya barabara ilikuwa hafifu sana lakini sasa katika kipindi hiki tumefanya mapinduzi makubwa mathalani kumekuwa na ongezeko la shule za msingi kufikia shule 64 toka 19 za awali”. Amefafanua Mhe. Mchengerwa 

Amesema eneo la Jimbo la Rufiji ni miongoni mwa maeneo yenye rutuba hapa nchini ambayo yanaweza kusitawisha mazao ya aina mbalimbali ambapo amefafanua kuwa katika miaka ya nyuma Rufiji lilikuwa eneo linazalisha pamba bora ukilinganisha na maeneo mengi.
Mhe. Mchengerwa anaendelea na mikutano ya hadhara katika kata nyingine za Jimbo hilo kuomba kura kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa madiwani na kwake mwenyewe ili apewe ridhaa ya kuwaongoza tena katika kipindi hiki.
Mhe. Mchengerwa ni Mbunge wa tisa wa kuchaguliwa katika jimbo hilo la Rufiji toka lianzishwe na kuongozwa na wabunge kadhaa kuanzia Mhe. Bibi Titi Mohamed ambapo anaelezewa kuwa ni miongoni mwa wabunge walioliletea maendeleo makubwa Jimbo hilo ukilinganisha na wabunge waliotangulia.
EmoticonEmoticon