TANESCO YAFANYA MATENGENEZO KINGA BILA KUZIMA UMEME NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME CHALINZE-KINYEREZI

September 04, 2025


📍*Ni kwa kutumia teknolojia ya Live Line*


📍*Wananchi waendelea kufurahia huduma ya umeme huku matengenezo yakiendelea*


Na Charles Kombe, Chalinze


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya matengenezo kinga kwenye njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti 220 kutoka Kituo cha kupoza umeme cha Chalinze hadi Kituo cha Kinyerezi Dar es Salaam bila kuzima umeme (live line).


Matengenezo hayo yalihusisha ubadilishaji wa vikombe (insulator) ambavyo vilionekana kuwa na changamoto katika ukaguzi uliofanywa kwenye njia hiyo ya kusafirisha umeme ambapo hapo awali ingelazimu kuzima umeme kwenye laini hiyo ambapo ingepelekea maeneo yanayopata umeme kupitia njia hiyo kukosa huduma kipindi cha matengenezo . 

Akingunzumza wakati wa zoezi hilo Mhandisi kutoka Kitengo cha usafirishaji umeme Philemon Tirukaizile alisema teknolojia hiyo  imeondoa kero ya kukatika umeme kwa wananchi wakati wa matengenezo. 

“Bila kuwa  na teknolojia hii  ya  kufanya matengenezo bila  kuzima  umeme, tungeweza  kuzima  njia yetu  ya kusafirisha umeme  kwa muda wa masaa sita. Ina  maana baadhi  ya wateja  wetu kuanzia hapa Chalinze kuelekea Mlandizi mpaka maeneo ya Kibaha 

wangeweza kukosa huduma ya umeme,” alisema Mha. Tirukaizile

Akifafanua namna wanavyotekeleza zoezi hilo, msimamizi wa timu ya usafirishaji Mkoa wa Pwani Bw. Sadiki Sadiki alieleza kuwa zoezi hilo linatekelezwa na mafundi wabobezi wenye mafunzo kwa kuzingatia usalama wa hali ya juu.


“Kabla hatujaanza kazi yetu huawa tunafanya mawasiliano ya watu wetu wa Kituo  cha kupoza umeme  ili waweze kupewa kibali cha  kufanya  zoezi  hili. Baada  ya hapo tunakua na kiongozi wa timu husika na  kila mmoja  anakuwa akizingatia usalama lakini kiongozi wa timu  ndiye   anatuma  maelekezo  nani afanye nini na wakati gani,” alieleza.  

Kwa upande wake Bi. Bahati Ramadhani ambae ni fundi katika kitengo hicho amesema ujuzi huo  ameupata kupitia mafunzo maalumu aliyoyapata ndani ya Shirika.


“Shirika  limenijenga   kwa   sababu  kabla  ya  kuanza  kazi  hii nilianza na mafunzo  kwenye msongo mkubwa  wa  njia  ya  kusafirisha umeme ya  Kilovoti 400 kutoka Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), na mafunzo yanaendelea. Kwa kweli ni fahari yetu mteja kuwa na umeme wakati wote,” aliongeza Bi. Bahati


 Teknolojia hii inalenga kupunguza upotevu wa umeme kutokana na kuzima laini pamoja na kuondoa malalamiko ya wateja wa maeneo husika ambao hapo awali walilazimika kukosa huduma ya umeme kwa muda ili kupisha matengenezo kinga.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »