Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Taifa na mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema kuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Geita Vijijini Joseph Kasheku Musukuma ni kiongozi mwenye sifa lukuki ikiwemo ya kusema ukweli na anayejua kuwasilisha shida za watu.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 15, 2025 wakati wa uzinduzi wa Kampeni katika Jimbo la Geita wilayani Geita mkoani Geita ikiwa ni kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29 mwaka huu.
Amesema moja ya ajenda ya Musukuma akiwa Bungeni ilikuwa kuhakikisha madini ya Geita yanapata thamani kwa ajili ya kunufaisha wananchi wa mkoa huo ambapo mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo ni kurejesha raslimali kwa wananchi wanaozunguka mgodi (CSR).
“ Miaka kadhaa Nkome haikuwa na umeme wala barabara lakini leo imebadilika kutokana na maendeleo yaliyopatikana. Hata halmashauri imekuja, Musukuma amejenga kituo cha polisi, nataka niwahakikishie kuwa Jakaranda watapata umeme, Musukuma anajua namna ya kufanyakazi na Rais Samia na anajua kusukuma maendeleo,” amesema Biteko.
Ameendelea kuwaeleza kampeni za mwaka huu ni maisha yao na maendeleo yao, Rais Samia anaipenda Geita ndio maana inajengwa lami kutoka Nzela kwenda Geita, Ushirombo , Katoro hadi Geita na maeneo mengine.
Amesisitiza “ Tumekuja leo kufungua kampeni nataka niwaambie kama mnahitaji leo kiongozi mmnaye, mbunge mnaye mimi nimefanya naye kazi anajua wapi pa kubonyeza ili mpate maendeleo, Musukuma kama ni mcheza mpira basi ni Pacome,”
Aidha, amewahimiza wananchi wa Jimbo la Geita Oktoba 29 kupiga kura na kumchagua mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgombea Ubunge kwa kuwa ili kuwa na maendeleo ni lazima viongozi hao washirikiane katika kutatua changamoto zao.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Nicholous Kasandamila amesema kuwa umati mkubwa wa wanachama wa CCM uliohudhuria mkutano huo unadhihirisha kuwa CCM imekubalika katika eneo hilo.
“Wingi huu niwape habari CCM tuliwaambia tutawaletea wagombea mnaowataka ninyi,” amesema Kasandamila.
Naye, Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Geita, Joseph Kasheku Musukuma amesema CCM ina utaratibu wa wagombea wengi na kumchagua mmoja hivyo amewashukuru wanachama wa CCM kwa kumchagua katika kura za maoni.
Amesema kuwa Nkome walikuwa na zahanati ambapo kila mwaka walikuwa wanazaliwa watoto kwa idadi kubwa hivyo Rais Samia alitoa fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha afya.
“ Tulikuwa tunakunywa maji ya ziwani, Rais Samia akatoa fedha sasa maji safi yanapatikana, Septemba 6 mwaka huu tumepokea fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya lami, haya ndo masuala yanayofanya watu wanaipenda CCM,” amesema Musukuma
Ametaja baadhi ya mafanikio ya Jimbo hilo kuwa barabara zote zinazounganisha kijiji kwa kijiji zinapitika. Aidha, walikuwa na shule nne za sekondari na sasa kwa kipindi cha miaka minne wana shule 34.
Sambamba na hayo amesema kuwa Serikali ya Rais Samia imewajengea shule ya amali na miradi mbalimbali na kusema kuwa wananchi hao wanahitaji kumshukuru kwa kumpigia kura.
Amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kuwapigia kura wagombea wote wa CCM.
Mwisho.
EmoticonEmoticon