Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) imechukua hatua mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa Miundombinu, kusimika mifumo bora ya TEHAMA na kushirikisha Wadau wa Sekta Binafsi wakiwemo waendeshaji wa Bandari, ili kuongeza ufanisi katika kuhudumia Shehena za ndani na nje ya nchi kupitia katika bandari za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mbossa wakati akifungua kikao cha Wadau wa Usafirishaji wa Shehena kupitia Ushoroba wa kati, Agosti 21, 2025 Kilichofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Naibu Mkurugenzi Mkuu Mha. Dkt. Baraka Mdima amesema, hatua hizi madhubuti zilichukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa na TPA kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha tija Bandarini, ziende sambamba na kujenga utamaduni wa Uadilifu na Uwajibikaji kwa Wafanyakazi wake, wateja na wadau ili kurahisisha ufanyaji biashara kupitia ushoroba wa kati.
Mha. Dkt. Mdima amesisitiza kuwa ni vyema, Wadau wanaoshiriki kikao hicho, wakajadiliana changamoto zinazokabili Sekta ya usafirishaji na kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kurahisisha biashara kupitia ushoroba wa kati.
Aidha, amewahakikishia Wadau wa Usafirishaji kuwa TPA inaendelea kuwa na dhamira ya dhati ya kuendelea kushirikiana na Wadau wake ili kuhakikisha kuwa Ushoroba wa Kati unakuwa wa kisasa, wenye ufanisi, na wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania na nchi zote zinazohudumiwa na ushoroba huo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Bw. Martin Masunga, amesema maoni yote yaliyotolewa na Wadau hao, yamepokelewa na yatafanyiwa kazi na Serikali ili kurahisisha ufanyaji wa Biashara na kuondoa ucheleweshaji kupitia Ushoroba wa kati.
Kikao hiki cha Wadau wa Usafirishaji kimeandaliwa na TPA chini ya Usimamizi wa Wizara ya Uchukuzi na kimehudhuriwa na Wadau mbalimbali wakiwemo Chama cha Mawakala wa Meli ( TASAA), Chama cha Mawakala wa Forodha ( TACAS) Baraza la Wasafirishaji ( TSC) Wamiliki wa Bandari Kavu ( CIDAT) Chama cha Wasafirishaji Tanzania ( TAT) na Chama cha Wamiliki wa Malori madogo na ya kati ( TAMSTOA).
EmoticonEmoticon